Mkurugenzi Mtendaji wa DUWASA, Mhandisi Aron Joseph, ameyasema hayo Oktoba 26, 2026, jijini Dodoma, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu changamoto mbalimbali zinazoikabili mamlaka hiyo, zikiwemo wizi wa mita za maji na mifuniko ya chemba za majitaka.
Amesema wizi na uharibifu wa miundombinu ya maji na majitaka unaweza kuongeza gharama za uendeshaji wa mamlaka hiyo, pamoja na kuhatarisha usalama wa wananchi na kuathiri utoaji wa huduma kwa jamii.
Aidha, Mhandisi Aron amesema takribani asilimia 70 ya wateja wa DUWASA wana mita za maji zilizofungwa ndani ya fensi za makazi yao, hali inayoweza kuleta changamoto katika usomaji wa mita kila mwezi na kurahisisha upatikanaji wa taarifa sahihi za matumizi ya maji.
Katika hatua nyingine, DUWASA imetoa tahadhari kuhusu wizi wa mifuniko ya chemba za majitaka, ikieleza kuwa kuondolewa kwa mifuniko hiyo kunaweza kusababisha ajali na kuhatarisha usalama wa watembea kwa miguu, waendesha pikipiki na madereva wanaotumia barabara hizo.
Kutokana na changamoto hizo, Mhandisi Aron amewataka wananchi kushirikiana na mamlaka hiyo kwa kutoa taarifa kwa DUWASA au Jeshi la Polisi wanapobaini vitendo vya wizi na uharibifu wa miundombinu ya maji na majitaka.
Amesisitiza kuwa ushirikiano wa wananchi ni muhimu katika kulinda miundombinu hiyo, kupunguza gharama zinazoweza kusababishwa na uharibifu na kuhakikisha huduma za majisafi na usafi wa mazingira zinaendelea kutolewa kwa ufanisi kwa wakazi wa Dodoma.




Comments
Post a Comment