KATIBU MKUU WIZARA YA AFYA NA MKURUGENZI MTENDAJI MUHIMBILI WAWEKA MIKAKATI MADHUBUTI KUBORESHA MFUMO WA MALIPO YA HUDUMA ZA AFYA
Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dkt. Grace Magembe, amekutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Dkt. Dellilah Kimambo, kwa lengo la kuimarisha utoaji wa huduma za afya na kuweka mikakati madhubuti ya kuboresha mfumo wa malipo ya huduma ili kuwawezesha wananchi kupata huduma kwa urahisi, haraka, kwa ufanisi na kuondoa malalamiko ya wananchi.
Katika kikao hicho, Dkt. Magembe amesisitiza umuhimu wa matumizi ya teknolojia katika kuboresha huduma za afya, akimtaka Mkurugenzi Mtendaji kuhakikisha mifumo ya TEHAMA ya hospitali inaendelea kuimarishwa ili kurahisisha mchakato wa malipo ya huduma, kuongeza uwazi kwa wananchi, kupunguza usumbufu na muda wa kusubiri kwa wagonjwa, pamoja na kuondoa udanganyifu.
“Mwananchi apate taarifa za malipo anayotakiwa kufanya kiganjani mwake kupitia simu ili kabla ya kulipa ajihakikishie kama malipo hayo ni sahihi au hapana”, amesema Dr Grace.
Amemwelekeza Mkurugenzi wa Muhimbili kuimarisha usimamizi wa huduma za afya kupitia viongozi walioko chini yake wakiwemo wakurugenzi, mameneja na wasimamizi wote na endapo kutakuwa na watumishi wowote wasiowajibika achukue hatua zilizo chini ya mamlaka yake na mengine yanayohitaji Wizara kufanyia kazi, ayawasilishe ili hatua stahiki zichukuliwe.
Amepongeza maboresho yanayoendelea kufanyika ikiwemo watumishi wanaofanya kazi kwa kujituma na weledi mkubwa.



Comments
Post a Comment