Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, ametembelea idara, vituo vya utafiti na maabara mbalimbali za Taasisi ya Teknolojia ya IIT Madras, jijini Chennai, nchini India leo tarehe 17 Julai, 2026.
Ziara hiyo imetoa fursa ya kujionea maendeleo yaliyofikiwa na Taasisi hiyo katika teknolojia, tiba, ubunifu na utafiti, pamoja na kubadilishana uzoefu kuhusu namna elimu, maarifa na teknolojia vinavyoweza kutumika kutatua changamoto za kiafya na kijamii.
Miongoni mwa maeneo aliyotembelea ni Kituo cha Sayansi ya Urithi, Kituo cha Taaluma na Tiba Asili za India, vituo vya utafiti wa sayansi na teknolojia za tiba, pamoja na Kituo cha Utafiti wa Kina wa Ubongo kwa kutumia Mbinu za Kisasa na Jumuishi za Anatomia ya Mfumo wa Neva. Aidha, ametembelea Maabara ya Anatomia na kujionea matumizi ya teknolojia za kisasa katika ufundishaji, uchunguzi na tafiti za afya.
Ziara hiyo inatarajiwa kufungua fursa zaidi za kuimarisha ushirikiano baina ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na IIT Madras, ambayo imeanzisha kampasi yake ya kwanza nchini Zanzibar. Ushirikiano huo unaunga mkono dhamira ya Serikali ya kuifanya Zanzibar kuwa kitovu cha elimu ya juu, teknolojia, utafiti na ubunifu katika ukanda wa Afrika.














Comments
Post a Comment