Na: Dawati la Habari, Polisi Mwanza.
Mtandao wa Polisi Wanawake Mkoa wa Mwanza (TPF-Net) umegusa maisha ya watoto wenye uhitaji maalum wanaolelewa katika Kituo cha Bustani C, Wilaya ya Sengerema, baada ya kutoa msaada wa chakula na mahitaji mbalimbali wenye thamani ya Sh milioni 3.685.
Msaada huo uliotolewa Oktoba 10, 2026, unalenga kupunguza changamoto za mahitaji ya kila siku kwa watoto hao, huku ukiimarisha uhusiano kati ya Jeshi la Polisi na jamii.
Akikabidhi msaada huo, Mkuu wa Mtandao wa Polisi Wanawake Mkoa wa Mwanza, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi, Virginia Sodoka, amesema wameamua kutembelea kituo hicho ili kuwafariji watoto na kuwapatia mahitaji muhimu.
Vifaa vilivyotolewa ni pamoja na mchele, sukari, mafuta ya kupikia, maharage, taulo za kike na vifaa vya shule.
Sodoka amesema msaada huo umegharamiwa kupitia michango ya maafisa, wakaguzi na askari wanawake wa vyeo mbalimbali wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza, ikiwa ni sehemu ya juhudi zao za kurudisha kwa jamii na kusaidia makundi yenye uhitaji.
Ameongeza kuwa matendo ya kijamii yana nafasi muhimu katika kujenga uaminifu na ushirikiano kati ya polisi na wananchi, hususan katika utoaji wa taarifa za uhalifu na wahalifu kwa ajili ya hatua za kisheria.Kwa upande wake, Sister Maria Rozei wa Shirika la Upendo Mtakatifu Kauli Bahomeo, aliyepokea msaada huo, ameishukuru TPF-Net kwa kuwajali watoto hao, akisema msaada huo utasaidia kukidhi mahitaji yao ya chakula na mahitaji mengine muhimu.
Naye Dorcas Ezilon, mmoja wa watoto wanaoishi katika kituo hicho, ameiomba jamii kuendeleza moyo wa kujitolea kwa kuwatembelea na kuwasaidia watoto wenye uhitaji maalum ili kuboresha maisha yao.
Hatua hiyo inaendelea kuonesha umuhimu wa ushirikiano kati ya taasisi za umma na jamii katika kusaidia makundi yenye uhitaji na kujenga jamii yenye mshikamano.





Comments
Post a Comment