Na: Dawati la Habari, Polisi Mwanza
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, DCP Wilbrod Mutafungwa, ameunga mkono juhudi za wananchi wa Kata ya Mkuyuni, jijini Mwanza, za kujenga upya kituo cha polisi kilichoharibiwa na kuchomwa moto wakati wa matukio ya Oktoba 29, 2025, akiwataka wananchi kushirikiana kulinda miundombinu ya umma ili kuzuia matukio kama hayo kujirudia.DCP Mutafungwa ameyasema hayo Oktoba 10, 2026, wakati wa mkutano wa hadhara uliofanyika Mkuyuni katika mwendelezo wa kampeni ya “Ongea na Kamanda”, ambapo amewahimiza wananchi kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa kituo hicho badala ya kuitegemea Serikali pekee.
Amesema Jeshi la Polisi liko tayari kutoa ramani na ushauri wa kitaalamu ili kuwezesha ujenzi huo, akisisitiza umuhimu wa kupata eneo lenye umiliki halali na lisilo na migogoro.
Ameeleza kuwa kukamilika kwa kituo hicho kutarahisisha upatikanaji wa huduma za kipolisi kwa wananchi wa Mkuyuni na maeneo jirani, pamoja na kuimarisha juhudi za kuzuia na kupambana na uhalifu. Aidha, amesisitiza umuhimu wa wananchi kulinda miundombinu ya umma ili kuepusha gharama za ziada zinazotokana na uharibifu na ujenzi upya.
Awali, Diwani wa Kata ya Mkuyuni, Richard Masesa, amesema kuungua kwa kituo cha polisi pamoja na ofisi ya kata kumesababisha wananchi kukabiliwa na changamoto ya kufuata huduma za kipolisi katika Kituo cha Polisi kilichopo eneo la Stendi Kuu ya Mabasi Nyegezi, umbali ulioongezeka kutokana na kukosekana kwa kituo hicho katika kata yao.
Masesa amesema tayari wameanza kuhamasisha wananchi kuchangia ujenzi huo na kushirikiana na wataalamu wa Jiji la Mwanza katika kutafuta eneo linalofaa kwa ajili ya ujenzi. Ameongeza kuwa wanatarajia kuitisha mkutano wa wadau ndani ya mwezi Oktoba ili kujadili na kuratibu hatua zinazofuata.
Pia, amemshukuru Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, CP Salim Hamduni, kwa kuunga mkono juhudi za kurejesha huduma hizo kupitia ujenzi wa kituo hicho.
Kwa upande wake, mkazi wa Mkuyuni, Adam Manyama, amewataka vijana kujiepusha na matumizi ya dawa za kulevya, ikiwemo bangi, pamoja na matumizi ya tumbaku na ugolo, akieleza kuwa tabia hizo zinaweza kuhatarisha afya na maisha yao.
Katika kuunga mkono juhudi hizo, DCP Mutafungwa ameahidi kuchangia matofali yenye thamani ya shilingi milioni moja kupitia ofisi yake kwa ajili ya kuanzisha ujenzi wa kituo hicho. Katika mkutano huo, mwananchi mmoja alichangia shilingi 50,000, huku mwingine akiahidi kuchangia mifuko ya saruji.
Akijibu hoja na kero zilizowasilishwa na wananchi, DCP Mutafungwa ameahidi kuratibu kikao na viongozi wa Vikundi vya Usimamizi wa Rasilimali za Uvuvi (BMU) kwa lengo la kujadili masuala ya usalama wa wavuvi na kutafuta namna ya kukabiliana na changamoto zinazowakabili.
Vilevile, amewataka wazazi na walezi kufuatilia kwa karibu mienendo ya watoto wao na kuwapa mwongozo unaofaa ili kuwakinga dhidi ya matumizi ya dawa za kulevya na vitendo vinavyoweza kuhatarisha maisha yao.








Comments
Post a Comment