Wananchi wa Kata ya Mabatini, Wilaya ya Nyamagana, mkoani Mwanza wamepongeza jitihada za Jeshi la Polisi kuwafikia vijana kwa njia ya michezo, hatua ambayo imesaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza matukio ya uhalifu kwenye kata hiyo. Pongezi hizo zimetolewa Septemba 13, 2025, wakati wa mashindano ya michezo yaliyoandaliwa na Jeshi la Polisi kupitia Mkaguzi Kata wa Mabatini. Mashindano hayo yalihusisha timu sita za mpira wa miguu kutoka mitaa sita ya kata hiyo ambazo ni; Mabatini Kusini, Mabatini Kaskazini, Majengo Mapya, Nyerere A, Nyerere B na Mbugani B. Katika mchezo wa fainali, timu ya Nyerere A iliibuka mshindi kwa kuifunga Majengo Mapya kwa mabao 2–1 na kukabidhiwa Mbuzi mmoja pamoja na zawadi nyingine. Akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhi zawadi kwa washindi, Kaimu Mkuu wa Polisi Wilaya ya Nyamagana Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP) Dastan Kombe, aliwataka wananchi na vijana waendelee kulipa kipaumbele suala la kulinda amani na usalama wa eneo lao. Alisema awali Kata...