Wananchi wa Kata ya Mabatini, Wilaya ya Nyamagana, mkoani Mwanza wamepongeza jitihada za Jeshi la Polisi kuwafikia vijana kwa njia ya michezo, hatua ambayo imesaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza matukio ya uhalifu kwenye kata hiyo.
Pongezi hizo zimetolewa Septemba 13, 2025, wakati wa mashindano ya michezo yaliyoandaliwa na Jeshi la Polisi kupitia Mkaguzi Kata wa Mabatini.
Mashindano hayo yalihusisha timu sita za mpira wa miguu kutoka mitaa sita ya kata hiyo ambazo ni; Mabatini Kusini, Mabatini Kaskazini, Majengo Mapya, Nyerere A, Nyerere B na Mbugani B.
Katika mchezo wa fainali, timu ya Nyerere A iliibuka mshindi kwa kuifunga Majengo Mapya kwa mabao 2–1 na kukabidhiwa Mbuzi mmoja pamoja na zawadi nyingine.
Akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhi zawadi kwa washindi, Kaimu Mkuu wa Polisi Wilaya ya Nyamagana Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP) Dastan Kombe, aliwataka wananchi na vijana waendelee kulipa kipaumbele suala la kulinda amani na usalama wa eneo lao.
Alisema awali Kata ya Mabatini ilikuwa na matukio mengi ya kihalifu, hata hivyo, kupitia juhudi za Mkaguzi Kata na ushirikiano wa wananchi, hali ya ulinzi na usalama imeimarika kwa kiasi kikubwa.
Kwa upande wake, Mkaguzi Kata wa Mabatini (Inspekta, Shaban Kashakala) alisema vijana wamebadilika na sasa ni mabalozi wa amani na usalama, jambo linalothibitisha mafanikio ya mkakati wa ushirikishwaji wa jamii katika ulinzi shirikishi.
Kwa upande wake, Nahodha wa timu ya Mzalendo, kwa niaba ya wachezaji wote, aliomba mashindano hayo ya michezo yaendelezwe, akibainisha kuwa michezo ni njia bora ya kuwaepusha vijana kujiingiza katika makundi ya kihalifu.
Naye, Daniel Nemes, ambaye ni Mkufunzi na Mwakilishi wa Kampuni ya Nchemi Investment Limited – Mwanza, alilipongeza Jeshi la Polisi kwa ubunifu wa kutumia michezo kama njia ya kuimarisha usalama. Aliahidi kutoa mafunzo ya ujasiriamali kwa vitendo bure kwa vijana waliokuwa washindi wa mashindano hayo.
*Kutoka: Dawati la Habari Polisi Mwanza*