Na Hamida Ramadhan, Rukwa
NAIBU Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora ambaye pia ni Mbunge wa Kwela, Mhe. Deus Sangu amewaomba Wananchi wasisahau maendeleo wanayoyaona katika Jimbo hilo ni kutokana na jitihada za Rais Mhe Dkt. Samia Suluhu Hassan kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Hayo ameyasema leo kwenye mkutano wa kampeni za Serikali za Mitaa uliofanyika katika Kijiji cha Ilemba, Kata ya Kalambanzite katika Jimbo la Kwela mkoani Rukwa.
Aidha, amefafanua kuwa ndani ya kipindi cha miaka mitatu ya Rais Mhe Dkt. Samia Suluhu Hassan, kata ya Kalambanzite imeimarika katika Sekta ya Afya, Elimu, Barabara, Maji pamoja na Umeme.
Amewataka Wananchi hao kujitokeza ifikapo Novemba 27 mwaka huu ili kuchagua Viongozi wenye maono na mwelekeo wa kuwaunganisha kuanzia ngazi ya shina hadi Taifa ambao ni Wagombea kupitia CCM.
" Chagueni Viongozi ambao wana uelewa wa matatizo na kujua namna ya kutatua changamoto zinazowakabili Wananchi pasipo kujali rangi, kabila au eneo, ” amesema Mhe. Sangu.
Mhe. Sangu amewaeleza Wananchi wa kata hiyo ya Kalambanzite kuwa wana kila sababu ya kuchagua Chama Cha Mapinduzi (CCM) chenye Sera zinazotekelezeka na kuachana na vyama vingine ambavyo sera zao zimelenga kuhubiri chuki na utengano.
“ Nimekuja kuwaomba mtuunge mkono kwa kupiga kura na kuchukua vijiji na vitongoji vyote, ” ameomba Mhe. Sangu.
Naye Mjumbe wa Kamati ya Siasa mkoa wa Rukwa, Patrick Maufi amewashukuru wagombea waliopitishwa na kusema hadi sasa CCM imesimamisha wagombea bila kupingwa katika ngazi mbalimbali katika uchaguzi huu.
Hata hivyo Mjumbe huyo amewataka Wananchi wakapige kura ya ndiyo kwa wagombea wa chama hicho waliopita bila kupingwa.






Comments
Post a Comment