MKUU wa Mkoa wa Mara, Mhe. Brigedia Jenerali Evans Alfred Mtambi, amewaelekeza Maafisa wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Operesheni Mafunzo, Kurugenzi ya Kukabiliana na Maafa, kutembelea na kufanya tathmini ya maeneo ya Bonde la Mto Mara katika Wilaya ya Serengeti, yanayokumbwa na mafuriko mara kwa mara.
Mhe. Mtambi ametoa maelekezo hayo leo, Oktoba 5, 2026, alipowapokea na kuzungumza na maafisa hao waliopo mkoani Mara kwa ziara ya kikazi yenye lengo la kutambua maeneo hatarishi yanayoweza kuathiriwa zaidi na mvua zinazotarajiwa kunyesha katika kipindi kijacho.
Akizungumza na maafisa hao, Mkuu huyo wa Mkoa amewakaribisha Mara na kuwahakikishia kuwa hali ya usalama mkoani humo ni shwari, huku wananchi wakiendelea na shughuli zao za kila siku bila hofu.
Hata hivyo, Mhe. Mtambi amewataka maafisa hao, pamoja na maeneo waliyopangiwa kuyatembelea, waongeze katika tathmini yao maeneo ya Bonde la Mto Mara, hasa katika Wilaya ya Serengeti, ambako wananchi wamekuwa wakikabiliwa na changamoto ya mafuriko kutokana na Mto Mara kuacha mkondo wake wa kawaida na kuvamia maeneo ambayo wananchi wanaishi na kufanya shughuli zao.
Amesema kutembelea maeneo hayo kutasaidia kubaini mapema maeneo yenye hatari na kuweka mikakati madhubuti ya kukabiliana na athari zinazoweza kujitokeza endapo mvua kubwa zitanyesha.
Mhe. Mtambi amesema maandalizi ya mapema ni muhimu katika kulinda maisha ya wananchi na mali zao, kwa kuwa utambuzi wa maeneo hatarishi kabla ya majanga kutokea unatoa nafasi kwa mamlaka kuchukua hatua za tahadhari na kujiandaa kwa ajili ya uokoaji pale inapohitajika.
Maafisa hao wa JWTZ wako mkoani Mara kwa ajili ya kufanya tathmini ya maeneo korofi yanayoweza kuathiriwa zaidi na mvua za El Niño zinazotabiriwa kuanza kunyesha hivi karibuni, hatua ambayo inalenga kusaidia Serikali kuwa na mpango wa maandalizi na mwitikio wa haraka katika kukabiliana na maafa.
Tathmini hiyo pia inatarajiwa kusaidia kubaini maeneo yanayoweza kuhitaji uangalizi maalumu, pamoja na kuweka utaratibu wa namna ya kusaidia kuokoa maisha ya wananchi na kulinda mali endapo kutatokea mafuriko au athari nyingine zinazohusiana na mvua kubwa.
Mkuu wa Mkoa amesisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya mamlaka za Mkoa, vyombo vya ulinzi na usalama pamoja na wananchi katika kuhakikisha tahadhari zinatolewa mapema na hatua zinazofaa zinachukuliwa kabla ya hali kuwa mbaya.

Comments
Post a Comment