WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba, amemwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika ibada ya kumuaga aliyekuwa Gavana wa kwanza wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Mzee Edwin Mtei, akimtaja kuwa kiongozi mahiri, mzalendo na nguzo muhimu katika historia ya uchumi na demokrasia ya Tanzania. Akizungumza katika ibada hiyo ya mazishi iliyofanyika nyumbani kwa marehemu Tengeru, Dkt. Nchemba alisema Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan anatambua mchango mkubwa wa marehemu kwa Taifa na Serikali mara zote itaenzi mchango wake mkubwa katika uchumi na demokrasia nchini. Waziri Mkuu alisema Mzee Mtei alikuwa miongoni mwa Watanzania wachache waliobahatika kuhudumu katika nyadhifa zote kuu za sekta ya fedha, ikiwemo kuwa Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Waziri wa Fedha na mwakilishi wa Tanzania katika taasisi za fedha za kimataifa, mchango uliompa heshima ya kipekee kitaifa na kimataifa. Alisema katika maisha yake ya utumishi wa u...