Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), amewasili Addis Ababa, Ethiopia, kushiriki kama mwanajopo katika Mazungumzo ya Mawaziri wa Fedha kuhusu ufadhili endelevu wa afya barani Afrika katika kipindi cha ufinyu wa bajeti na juhudi za nchi kujitegemea katika masuala ya afya.
Mhe. Omar amepokea taarifa kuhusu maandalizi ya ushiriki wake na agenda za mkutano huo kutoka kwa Kaimu Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, ambaye pia ni Kamishna wa Idara ya Fedha za Nje, Bw. Rished Bade, katika Ofisi za Ubalozi wa Tanzania nchini Ethiopia.
Mazungumzo hayo yanawakutanisha Mawaziri wa Afya na Fedha, washirika wa maendeleo na viongozi wa kikanda kujadili changamoto za kifedha zinazoathiri upatikanaji wa huduma za afya kwa wote (UHC), ikiwemo kupungua kwa misaada kutoka nje, ufinyu wa bajeti na kuongezeka kwa mzigo wa madeni.
Mkutano huo unafanyika kabla ya Kikao cha 76 cha Kamati ya Kanda ya Shirika la Afya Duniani (WHO) kwa Afrika.

Comments
Post a Comment