Wabunge mbalimbali wameipongeza Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuimarisha amani, usalama na heshima ya nchi ndani na nje ya mipaka yake.
Akichangia makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa kwa mwaka wa fedha 2026/2027 Bungeni jijini Dodoma, Mbunge wa Jimbo la Kisarawe, Selemani Jafo amesema Tanzania imeendelea kuwa kisiwa cha amani kutokana na uongozi imara wa Rais Samia pamoja na uwekezaji mkubwa katika sekta ya ulinzi na usalama.
Jafo amesema uimara wa vyombo vya ulinzi na usalama umeiwezesha Tanzania kuheshimika kimataifa, huku Jeshi la Wananchi wa Tanzania likiendelea kuwa nguzo muhimu katika kulinda amani ndani na nje ya bara la Afrika.
“Rais Samia ameonesha dhamira ya dhati ya kuhakikisha Tanzania inaendelea kuwa salama, tulivu na kuheshimika kimataifa kupitia uimarishaji wa sekta ya ulinzi na usalama,” amesema Jafo.
Katika mchango wake, amempongeza Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Rhimo Nyansaho kwa uongozi wake aliouonesha tangu alipoteuliwa, akisema amedhihirisha weledi, mshikamano na ushirikiano ndani ya wizara na taasisi zake.
Aidha, amempongeza Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Tanzania, Jacob Mkunda pamoja na uongozi wa wizara ikiwemo Katibu Mkuu Faraji Mnyepe kwa kuendelea kuimarisha nidhamu, weledi na ufanisi ndani ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).
Kwa upande wake, Mbunge wa Ikungi Magharibi, Elibariki Kingu amesema uimara wa JWTZ umeendelea kuwa msingi wa amani na mshikamano wa taifa, akisisitiza kuwa bila amani hakuna maendeleo ya kweli yanayoweza kupatikana.
Kingu amesema viongozi wenye unyenyekevu na nidhamu wamekuwa chachu ya kuimarika kwa taasisi za ulinzi na usalama, huku akitoa wito kwa wananchi kuendelea kuiunga mkono Serikali na vyombo vya ulinzi.
Naye Mbunge wa Viti Maalum (Vijana), Zainab Abdallah Issa amevipongeza vyombo vya ulinzi na usalama kwa kazi kubwa ya kulinda amani ya taifa, akisema mchango wao umeendelea kuwa nguzo muhimu ya utulivu wa Watanzania wote.
Amesema wakati wananchi wakiendelea na shughuli zao za kila siku, vyombo hivyo vinafanya kazi usiku na mchana kuhakikisha nchi inabaki salama.
“Tunapaswa kuendelea kuviunga mkono vyombo vyetu vya ulinzi na usalama kwa kazi kubwa vinayoifanya ya kuhakikisha Tanzania inaendelea kubaki salama wakati wote,” amesema Zainab.
Wabunge hao kwa pamoja wamesisitiza kuwa amani na usalama ni msingi wa maendeleo ya taifa, wakitoa wito wa kuendelea kuimarishwa kwa sekta ya ulinzi na mshikamano wa kitaifa.








Comments
Post a Comment