WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Dkt. Ashatu Kijaji amesema Serikali imeendelea kuimarisha vita dhidi ya ujangili na biashara haramu ya nyara kupitia matumizi ya teknolojia, mafunzo ya kisasa kwa maafisa wa uhifadhi pamoja na ushirikiano wa kimataifa katika kulinda rasilimali za wanyamapori nchini.
Akiwasilisha bajeti ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa mwaka wa fedha 2026/2027 leo Mei 15, 2026 bungeni jijini Dodoma, Dkt. Kijaji amesema Serikali kwa kushirikiana na United Nations Development Programme kupitia ufadhili wa Mfuko wa Dunia wa Mazingira (GEF), inaendelea kutekeleza Mradi wa Kukabiliana na Ujangili na Biashara Haramu ya Nyara nchini kwa lengo la kuimarisha ulinzi wa maliasili na kudhibiti mtandao wa wahalifu wa wanyamapori.
Amesema katika mwaka wa fedha 2025/2026, zaidi ya Sh bilioni 2.58 ziliidhinishwa kwa utekelezaji wa mradi huo ambapo hadi Aprili 2026 kiasi cha Sh bilioni 1.32 tayari kilikuwa kimetolewa kwa ajili ya shughuli mbalimbali za kuimarisha operesheni za uhifadhi nchini.
“Mradi huu umewezesha mafunzo ya uchunguzi wa kisayansi kwa maafisa wa Kikosi Kazi Taifa Dhidi ya Ujangili (NTAP), Idara ya Wanyamapori, Kanda za Kiikolojia za Kuratibu Doria pamoja na Jeshi la Uhifadhi wa Wanyamapori na Misitu ili kuongeza uwezo wa kukabiliana na uhalifu wa wanyamapori,” amesema Dkt. Kijaji.
Amesema Serikali pia imeendelea kuimarisha ushirikiano wa kikanda kupitia doria za pamoja kati ya Tanzania na Zambia katika mpaka wa Tunduma/Nakonde pamoja na operesheni za pamoja kati ya Tanzania na Kenya katika mifumo ikolojia ya Serengeti-Mara na Tsavo-Mkomazi kwa lengo la kudhibiti njia za biashara haramu ya nyara mipakani.
Kwa mujibu wa Dkt. Kijaji, mradi huo umeongeza matumizi ya mifumo ya kisasa ya kubadilishana taarifa za uhalifu wa wanyamapori ikiwemo WITIS na EAC-TWIX, hatua inayowezesha maafisa wa Tanzania kushirikiana kwa karibu zaidi na wenzao kutoka Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi na DRC katika kubaini na kufuatilia mitandao ya wahalifu.
Aidha, maafisa 81 kutoka Idara ya Wanyamapori na Kanda za Kiikolojia za Kuratibu Doria wamepatiwa mafunzo kuhusu uchunguzi wa maeneo ya uhalifu, uchambuzi wa uhalifu wa mtandao na ukusanyaji wa sampuli kwa ajili ya uchunguzi wa kisayansi.
Serikali imedhamiria kuimarisha doria za kiintelijensia, matumizi ya teknolojia na ushirikiano wa kikanda ili kuhakikisha rasilimali za Taifa zinalindwa dhidi ya vitendo vya ujangili na biashara haramu ya nyara.







Comments
Post a Comment