MwanaFA awasilisha majibu ya haki za wasanii kwa Kamati ya bunge

GEORGE MARATO TV
0


Na Mashaka Mhando, Dodoma

NAIBU Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Hamis Mwinjuma (MwanaFA), leo ameongoza ujumbe wa Wizara mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo kuwasilisha na kujadili majibu ya hoja za Bunge kuhusu Sheria ya Haki ya Kunufaika na Mauzo Endelevu (Resale Right) ya mwaka 2025.

Uwasilishaji huo wa leo, Machi 25, 2026, unalenga kutoa ufafanuzi wa kina juu ya kanuni na taratibu zitakazomwezesha msanii wa Tanzania kuendelea kupata mirabaha (Royalty) kila mara kazi yake inapouzwa tena sokoni na mtu mwingine baada ya mauzo ya awali.

Akizungumza mbele ya Kamati hiyo jijini Dodoma, Mhe. Mwinjuma amebainisha kuwa Wizara imefanyia kazi hoja zote zilizoibuliwa na Bunge ili kuhakikisha sheria hiyo ndogo inakuwa na tija na inatekelezeka bila vikwazo kwa wadau wa kazi za sanaa na ubunifu.

Mhe. Naibu Waziri ameeleza kuwa Wizara imefanya uchambuzi wa kina wa hoja za Bunge ili kuhakikisha sheria hiyo ndogo inakidhi vigezo vya kisheria na inatekelezeka bila kuleta urasimu kwa wadau wa sanaa na michezo.

“Tumejadili kwa kina na Kamati ya Bunge kuhusu namna bora ya kusimamia haki hizi za mauzo endelevu. Lengo la Serikali ya Awamu ya Sita ni kuhakikisha msanii ananufaika na jasho lake maisha yake yote, hata baada ya kuuza kazi yake kwa mara ya kwanza,” amesema Mhe. Mwinjuma na kuongeza,

"Tumeitikia wito wa Kamati na kuwasilisha majibu ya hoja mbalimbali kuhusiana na Resale Right. Lengo letu ni kuhakikisha msanii ananufaika na jasho lake hata baada ya kazi yake kupanda thamani huko sokoni,”

Sheria hiyo ya Resale Right ya mwaka 2025 inatajwa kuwa mkombozi wa wasanii wa michoro, sanamu na kazi nyingine za mikono, ambapo awali walikuwa wakikosa mapato pindi kazi zao zilipouzwa kwa bei kubwa na madalali au wamiliki wa maghala ya sanaa (Art Galleries).

Utekelezaji wa kanuni hizi za Resale Right unatajwa kuwa ni mapinduzi makubwa katika sekta ya utamaduni na sanaa, kwani Tanzania inakuwa miongoni mwa nchi zinazopiga hatua kubwa katika kulinda miliki bunifu kulingana na mabadiliko ya soko la kimataifa.

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo imepokea majibu hayo na kutoa mapendekezo ya namna ya kuboresha zaidi mifumo ya ukusanyaji na usambazaji wa miraba hiyo ili kusiwe na mianya ya upotevu wa mapato kwa wasanii.

Wizara imesisitiza kuwa maboresho hayo yamezingatia mazingira ya sasa ya biashara ya sanaa ndani na nje ya nchi, huku yakilenga kuongeza mchango wa sekta ya utamaduni na sanaa katika Pato la Taifa (GDP).






Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
Post a Comment (0)

#buttons=(Accept !) #days=(20)

Our website uses cookies to enhance your experience. Learn More
Accept !
To Top