Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan amewaomba Viongozi wa kimila, Machifu, Watemi na Watanzania kwa Ujumla kuendelea kuliombea Taifa amani na utulivu wakati huu ambapo nchi inajiandaa kushiriki Uchaguzi Mkuu Mwezi Oktoba Mwaka huu.
Rais Samia pia amekemea vikali ramli chonganishi kwenye Jamii hasa kwenye mchakato wa uchaguzi Mkuu, akieleza kuwa wanaowania nafasi mbalimbali za Uongozi watakuwa wageni wa waganga wa Kienyeji, hivyo ni muhimu kutanguliza maslahi ya Taifa mbele kwa kudumisha amani na utulivu nchini.
Rais Samia ameyasema hayo alipokuwa akihutubia maelfu ya wananchi walioshiriki kwenye Tamasha la kitamaduni la Bulabo, linalohusisha Jamii ya Kisukuma kutoka Mikoa ya Kanda ya ziwa.
Tamasha linalitarajiwa kufikia kilele chake Jumapili Juni 22, 2025 kwa Ibada itakayoongozwa na Kanisa Katoliki Mkoani Mwanza, Misa ikitarajiwa kuongozwa na Mhashamu Baba Askofu Renatus Nkwande wa Jimbo kuu la Mwanza.
"Waganga wale wa kienyeji, Ombi langu kwenu kipindi hiki wanaoomba kupata nafasi mbalimbali watawatembelea na wanapowatembelea niombe sana tusifanye ramli chonganishi kwasababu hizo ndizo zinazovunja amani kwenye uchaguzi. Kama anakuja na fungu, we kula fungu umemuona atashinda, mwambie utashinda, umemuona hatashinda mwambie Baba wewe nenda tu mambo mazuri. Kula pesa yako nenda kalale, lakini tusifanye ramli chonganishi kwamba naona kama utashinda lakini kuna Katibu wako huyu wa Mkoa kama hakupendipendi hivi, hapana, tufanye mambo kwa murua ili watu wote waende vizuri, tumalize vizuri." Amesema Rais Samia.














Comments
Post a Comment