Soko la Mbao la Sabasaba Manispaa ya Ilemela Jijini Mwanza limeteketea kwa Moto usiku wa Kuamkia Machi 17 mwaka huu.
Kuteketea kwa soko hilo kumeathiri zaidi ya wafanyabiashara 30 ambao Mali zao ambazo thamani yake bado haijajulikana zimeteketea kwa moto.
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Said Mtanda leo Machi 17,2025 amewatembelea wafanyabiashara wa mbao wa Soko la Sabasaba na kuwapa pole pamoja na kuwaomba kuwa na utulivu wakati taarifa ya uchunguzi wa chanzo cha moto huo ikiendelea kufanyika.
Mtanda amesema kuwa mara baada ya taarifa ya Uchunguzi kukamilika na kusomwa, Ofisi yake itakutana na wafanyabiashara hao pamoja na taasisi za fedha ili kuona namna ya kuwapa muda zaidi wa marejesho ya fedha kwa wale waliokopa.
"Natoa rai kwa vyombo vya dola kuharakisha uchunguzi huu ili kutambua chanzo na kujua nini kifanyike na wafanyabiashara hao waendelee na shughuli zao mapema iwezekanavyo kama Serikali inavyohimiza wananchi kuwajibika",Mtanda
Aidha amewataka wafanyabiashara hao kuzingatia matumizi ya vifaa vya kuzimia moto na bima ambayo itawasaidia kuepuka hasara kubwa yanapotokea majanga ya moto.
Amebainisha mara baada ya kutembelea maeneo yaliyoathirika na moto huo amepata taarifa idadi kubwa hawatumii vifaa vya kuzimia moto licha ya elimu ya matumizi hayo kutolewa mara kwa mara na Jeshi la zimamoto na uokoaji.
"Serikali kuna maeneo ya majanga inawajibika moja kwa moja kuwagharamia wananchi na mengine haiwajibiki nayo kama hili,narudia kuwakumbusha kuzingatia sheria zinavyotaka ili kujihakikishia usalama wa muda wote wa mali zenu,niwapongeze pia Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kwa kufanya kazi hii kwa weledi na kuokoa sehemu kubwa ya mali za wafanyabiashara hawa,"mkuu wa mkoa
Kwa upande wake kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Mwanza SSF Elisa Kamugisha amebainisha moto huo ulianza majira ya saa saba usiku na kufanikiwa kwa asilimia kubwa kuwahi kuuzima usienee sehemu nyingine.
"Hapa kuna wafanyabiashara wa mbao zaidi ya elfu moja lakini walioathirika na janga la moto ni thelathini,lakini taarifa rasmi itatolewa muda siyo mrefu"SSF Kamugisha.





.jpg)
.jpg)
.jpg)
.jpg)
.jpg)
.jpg)
.jpg)
.jpg)






Comments
Post a Comment