Na Wellu Mtaki, Geita
BODI ya Bima ya Amana (DIB) imewataka wananchi kuepuka kuhifadhi fedha nyumbani na badala yake kutumia huduma za benki na taasisi za fedha zilizoidhinishwa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT), ikieleza kuwa hatua hiyo inalinda fedha zao na kuchangia katika kukuza shughuli za kiuchumi.
Meneja wa Fedha na Uhasibu wa DIB, Romuli Mtui, amesema hayo wakati wa Maonesho ya Tisa ya Kitaifa ya Teknolojia ya Madini yanayoendelea mkoani Geita, ambapo Bodi hiyo inatoa elimu kwa wananchi kuhusu huduma za kifedha na mfumo wa bima ya amana.
Mtui amesema kuhifadhi fedha nyumbani kunaweza kumuweka mwananchi katika hatari ya kuzipoteza kutokana na matukio mbalimbali, ikiwemo wizi, moto au mafuriko.
“Fedha zinapokuwa nyumbani hazishiriki kikamilifu katika mzunguko wa uchumi. Lakini zinapowekwa katika taasisi za fedha, zinaweza kutumika katika shughuli mbalimbali, ikiwemo kuwa sehemu ya mikopo inayowawezesha wananchi na wafanyabiashara kupata mitaji,” amesema.
Amesema wananchi wanaoweka fedha zao katika benki na taasisi za fedha zilizo katika mfumo wa bima ya amana hunufaika na kinga hiyo bila kulazimika kujisajili binafsi wala kulipa mchango wa ziada.
Kwa mujibu wa DIB, bima ya amana hutofautiana na bima nyingine ambazo mteja anatakiwa kujisajili na kulipa ada au michango ili kupata kinga.
Imeelezwa kuwa endapo benki au taasisi ya fedha itashindwa kuendelea na shughuli zake kutokana na kufilisika, Mfuko wa Bima ya Amana hutumika kulipa fidia kwa wateja kwa mujibu wa taratibu na kiwango kinachotambuliwa kisheria.
Bodi hiyo imeeleza kuwa Mfuko wa Bima ya Amana ulianzishwa mwaka 1994, wakati DIB ilipoanza shughuli zake rasmi, na umeendelea kukusanya michango kutoka kwa wanachama wake ambao ni benki na taasisi za fedha.
Aidha, kwa mujibu wa maelezo ya Bodi hiyo, chini ya Sheria ya Benki na Taasisi za Fedha ya mwaka 2006, benki na taasisi za fedha zinatakiwa kuchangia katika Mfuko wa Bima ya Amana.
Fedha za mfuko huo huwekezwa katika maeneo salama, ikiwemo hati fungani za Serikali, huku mapato yatokanayo na uwekezaji huo pamoja na michango ya wanachama yakisaidia kuongeza uwezo wa mfuko kulipa fidia pale taasisi ya fedha inapofilisika.
Bodi hiyo pia imeeleza kuwa ina nafasi katika kushughulikia changamoto zinazoweza kuzikabili benki au taasisi za fedha kabla hazijafikia hatua ya kushindwa kuendelea na shughuli zake.
Kwa mujibu wa maelezo hayo, Benki Kuu ya Tanzania, ambayo ndiyo msimamizi wa benki na taasisi za fedha, inaweza kuihusisha DIB katika kutafuta njia mbalimbali za kushughulikia taasisi inayokabiliwa na changamoto kwa lengo la kulinda amana za wateja na kupunguza gharama kwa Mfuko wa Bima ya Amana.
Imeelezwa kuwa hatua hizo hufanyika baada ya kutathmini hali ya taasisi husika na kubaini njia yenye gharama nafuu zaidi kwa mfuko, huku kipaumbele kikiwa ni kulinda amana za wananchi.
Katika maelezo yake, DIB imetaja takwimu za Juni 30, 2022, ambazo zilionyesha kuwa kulikuwa na zaidi ya akaunti milioni 49.5 za amana katika benki, huku asilimia 98 ya akaunti hizo zikiwa zinapata kinga ya bima ya amana kwa asilimia 100.
Bodi hiyo imesema elimu inayotolewa katika Maonesho ya Teknolojia ya Madini inalenga kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu mfumo wa bima ya amana, usalama wa fedha zao na umuhimu wa kutumia huduma rasmi za kifedha badala ya kuhifadhi fedha nyumbani.

Comments
Post a Comment