Na Wellu Mtaki, Geita
WACHIMBAJI wa madini mkoani Geita wametakiwa kutumia vipimo vya kisayansi kubaini aina na kiwango cha madini katika sampuli zao badala ya kutegemea rangi ya mawe au mwonekano wa madini kwa kutumia darubini pekee.
Ushauri huo umetolewa na wataalamu wa maabara ya madini ya NJEMA GEOCHEMICAL LABORATORY ambao wamesema matumizi ya teknolojia na uchambuzi wa kisayansi yanaweza kuwasaidia wachimbaji kufanya maamuzi sahihi kabla ya kuwekeza fedha zaidi katika uchimbaji.
Wataalamu hao wamesema,baadhi ya wachimbaji wamekuwa wakifanya maamuzi kwa kuangalia rangi ya jiwe au dalili za madini zinazoonekana kwa macho, jambo ambalo haliwezi kutoa uhakika wa kiwango halisi cha madini kilichopo kwenye sampuli.
“Tunachofanya ni kuwasaidia wachimbaji wadogo na wa kati kufanya maamuzi sahihi kwa kutumia taarifa za kisayansi za kimaabara.Hii inamsaidia mchimbaji kujua kwa uhakika sampuli yake ina madini gani na kwa kiwango gani,” wamesema.
Pia wataalamu hao wamesema maabara hiyo inayopatikana mtaa wa Nyamalembo, Barabara ya kwenda mgodibwa dhahabu wa Geita (GGM).Chunya wanapatikana mtaa Kibaoni,na kwa Kahama wanapatikana mtaa wa Mbulu -Isaka Road.
Kwa mujibu wa wataalamu hao, mchakato wa kutafuta na kuthibitisha uwepo wa madini unapaswa kuhusisha utafiti, uchukuaji sahihi wa sampuli na uchambuzi wa maabara kabla ya kufanya maamuzi makubwa ya uwekezaji.
Sampuli zipimwe hata baada ya mlipuko
Wataalamu wa NJEMA LABS wamesema hata baada ya kufanya ulipuaji wa miamba katika eneo la uchimbaji, wachimbaji wanapaswa kuchukua sampuli na kuzipeleka maabara kwa ajili ya uchunguzi badala ya kutegemea mwonekano wa mawe yaliyolipuliwa.
Wameongeza kusema,sampuli inayowasilishwa maabara inapaswa kuwa kiwakilishi sahihi cha eneo linalochunguzwa ili matokeo yatakayopatikana yaweze kusaidia katika kufanya maamuzi.
“Ni muhimu kuhakikisha sampuli inayokuja maabara inawakilisha eneo linalochunguzwa. Sampuli inaweza kuhitaji kuvunjwa na kusagwa kwa utaratibu maalumu ili kupata matokeo yanayoweza kutumika katika kufanya maamuzi,” wamesisitiza wataalamu hao.
Wameongeza kuwa maabara hiyo hutumia mbinu mbalimbali za kiuchunguzi wa sampuli.
“Rangi ya jiwe si uthibitisho wa dhahabu”
Aidha, wataalamu hao wameonya dhidi ya dhana kwamba rangi au mwonekano wa jiwe pekee hauwezi kuwa uthibitisho wa uwepo wa kiwango kikubwa cha dhahabu.
Wamesema mchimbaji anaweza kuona jiwe na kudhani lina kiwango kikubwa cha dhahabu, lakini baada ya kufanyiwa uchunguzi wa maabara akabaini kuwa kiwango cha madini hayo ni kidogo au hakipo kwa kiwango alichotarajia.
“Unaweza kuona jiwe na ukadhani ni dhahabu, lakini bila kufanya uchambuzi wa kisayansi huwezi kujua kwa uhakika kiwango kilichopo. Ndiyo maana tunashauri watu wapime sampuli zao kabla ya kufanya maamuzi makubwa,” wamesema.
Kwa hiyo, wachimbaji na wafanyabiashara wa madini wametakiwa kutumia matokeo ya vipimo vya maabara kama sehemu ya taarifa muhimu wakati wa kufanya maamuzi kuhusu ununuzi wa sampuli, uchimbaji au uwekezaji katika maeneo yenye viashiria vya madini.
Maabara hiyo pia inatoa huduma katika maeneo mbalimbali, yakiwemo Geita,Kahama na Chunya. Kwa Geita, kituo hicho kinapatikana Nyamalembo, Barabara ya kwenda mgodi wa dhahabu Geita(GGM).
Wataalamu hao wamesema matumizi ya teknolojia na vipimo vya maabara katika sekta ya madini ni muhimu katika kuongeza ufanisi wa shughuli za uchimbaji na kupunguza maamuzi yanayotokana na makadirio yasiyothibitishwa kisayansi.



Comments
Post a Comment