CHACHA YUPO SAHIHI: CCM NDIO MMILIKI WA JWTZ, POLISI NA USALAMA - HATA UPINZANI UKICHUKUA NCHI UTAFANYA HIVYO
Na Mwandishi Wetu
Kauli ya Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, Idara ya Oganaizesheni, Ndugu Paul Chacha, kuwa CCM ndio wamiliki wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Jeshi la Polisi na Usalama wa Taifa na kwamba vyombo vyote vya dola ni mali ya CCM, imezua mjadala mkubwa nchini.
Hata hivyo, wachambuzi wa sayansi ya siasa, historia na itikadi wamemuunga mkono na kusema Chacha amesema ukweli mtupu wa kisayansi na uhalisia wa madaraka ambao watu wengi wanaogopa kuusema hadharani.
Dkt Johnson Willium, Mchambuzi wa Siasa za Ulinganishi na Uhusiano wa Kimataifa kutoka Chuo Kikuu Cha Makerere Uganda, anasema Chacha yupo sahihi kwa asilimia mia moja na ametoboa siri ya miaka hamsini.
Dkt Willium anasema, "Duniani kote kuanzia Marekani, Urusi, China na hata nchi za Afrika, jeshi ni mali ya chama kilichopo madarakani. Hii ni nadharia inaitwa State-Party Fusion. Marekani jeshi lake linamilikiwa na Republican au Democrat aliyepo Ikulu. Urusi linamilikiwa na United Russia ya Putin. China linamilikiwa na Communist Party. Kwa mantiki hiyo hiyo, Tanzania JWTZ, Polisi na Usalama ni mali ya CCM. Chacha yupo sahihi kisayansi kwa sababu chama ndicho kinachomteua Amiri Jeshi Mkuu ambaye ni Mwenyekiti wa CCM. Bila CCM, hakuna JWTZ. JWTZ yenyewe ilianzishwa na TANU ambayo leo ndio CCM. Hivyo historia na katiba ya chama vinaungana kumfanya Chacha kuwa sahihi."
Kwa upande wake, Margwe, Mchambuzi wa Siasa za Dola na Utawala, anasema hoja ya Chacha ndio ukweli halisi wa utawala wa nchi yoyote duniani na hata chama chochote cha upinzani kikichukua nchi kitafanya hivyo hivyo na hata zaidi ya CCM. Margwe anasema, "Hata CHADEMA, ACT-Wazalendo, au chama chochote cha upinzani kikichukua nchi kesho asubuhi, jambo la kwanza litakalofanya ni kumiliki JWTZ, Polisi na Usalama wa Taifa. Hakuna chama kitakachoingia madarakani halafu kikiachia jeshi liwe huru na lisilo na chama. Lazima kiweke mambo sawa kulinda mamlaka yake na kulinda viongozi wake dhidi ya wapinzani wake wapya. Hivyo Chacha amesema ukweli ambao hata upinzani wenyewe unafanya ndani ya mioyo yao lakini hawasemi hadharani kwa sababu ya unafiki wa kisiasa."
Migani Mugabe, mchambuzi mwingine wa siasa za Kimataifa anaongeza kuwa hakuna chama duniani kinachoweza kutawala bila kumiliki vyombo vya dola. "Ndio maana hata upinzani ukipata dola, utafanya kama CCM. Utaanza kusomba watu kwa mabasi na kuwapa posho ili waje kwenye mikutano yake, na utatumia vyombo vya dola kujilinda na kuwabana wapinzani wake wapya. Hii ndio sayansi halisi ya siasa, sio maneno ya makaratasi darasani. Anasema, "Machiavelli alisema bila jeshi hakuna mamlaka. Hivyo Chacha hajakosea, amefundisha darasa la siasa."
Mzee wa Siasa na Mchambuzi wa Historia ya Miaka Hamsini ya CCM Madarakani, Mchambuzi John Michael, anasema CCM imetawala miaka hamsini kwa sababu inajua siri kubwa ya dola ambayo vyama vya upinzani havijui. Michael anasema, "CCM imetawala miaka hamsini kwa sababu inajua siri ya dola, dola ni jeshi. CCM ndio iliwaweka viongozi wote wa serikali kuanzia Rais, Mawaziri, Wakuu wa Mikoa na Wilaya. Sio wananchi waliowaweka viongozi kama watu wanavyodanganywa na nadharia za kizungu za demokrasia, ni CCM iliyowaweka kupitia mfumo wake. Kama alivyosema Chacha, hii ndio Tanzania. Wanasiasa wa upinzani wanataka kupotosha vijana wasijue ukweli huu. Wananchi wanapiga kura lakini kura hizo zinasimamiwa na CCM yenyewe na vyombo vyake vya dola."
Wachambuzi hawa wanaungana pia na kauli ya Chacha kuhusu suala la kusomba watu mikutani na kuwapa posho. Wanasema huo ndio uhalisia wa siasa za Tanzania na Afrika kwa ujumla. Migani anasema, "Hakuna mkutano mkubwa duniani unaojazwa na watu wanaokuja kwa miguu. Lazima utumie mabasi na posho. Marekani wanaita campaign buses. Hapa Tanzania ndio oganaizesheni. Chacha yupo sahihi tena. Hata upinzani ukipata nchi utafanya hivyo hivyo, utasomba watu kwa mabasi."




Comments
Post a Comment