Na Wellu Mtaki, Geita
KAMPUNI inayojihusisha na uuzaji wa vifaa na utoaji wa huduma za kitaalamu katika sekta ya uchimbaji imeanza kutumia teknolojia mpya za milipuko zinazolenga kuwasaidia wachimbaji kukabiliana na changamoto za mazingira na kufikia maeneo ambayo awali yalikuwa magumu kufikika.
Teknolojia hiyo, ikiwamo matumizi ya mashine za MMU, imeelezwa kuwa inaweza kutumika katika mazingira yenye kiwango kikubwa cha maji, hivyo kuwapa wachimbaji fursa ya kutumia teknolojia inayolingana na mazingira ya eneo husika.
Afisa Masoko wa ESEH INVESTMENTS, William Sisty, amebainisha hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari katika Maonesho ya Tisa ya Madini yanayofanyika mkoani Geita, mara baada ya kampuni hiyo kutembelewa na Mkuu wa Wilaya ya Chato.
Sisty amesema kampuni hiyo, ambayo imekuwa ikitoa huduma tangu mwaka 2014, imeendelea kuwekeza katika teknolojia na vifaa vya kisasa ili kukidhi mahitaji ya wachimbaji wadogo, wa kati na wakubwa.
“Tumekuwa tukijikita katika kuwahudumia wachimbaji wadogo, wa kati na wakubwa, huku tukiendelea kuendana na mabadiliko ya teknolojia katika sekta ya uchimbaji,” amesema Sisty.
Amesema matumizi ya mashine na vifaa vya kisasa yanaweza kusaidia kupanua wigo wa huduma za kampuni hiyo, hususan katika maeneo yenye changamoto za kimazingira yanayohitaji teknolojia maalumu.
Mbali na uuzaji wa vifaa, kampuni hiyo pia imepanua huduma zake kwa kutoa utaalamu wa kiufundi kwa wachimbaji ambao wana vifaa lakini hawana timu yenye utaalamu wa kufanya tathmini ya eneo na kuandaa mipango ya milipuko.
Kwa mujibu wa Sisty, kampuni hutoa timu za wataalamu wa kiufundi wanaosaidia wachimbaji katika shughuli mbalimbali zinazohitaji utaalamu maalum
Hatua hiyo inalenga kuwawezesha wachimbaji kutumia vifaa walivyonavyo kwa ufanisi zaidi, huku wakizingatia mahitaji ya eneo husika na taratibu za usalama katika shughuli za uchimbaji.
Kampuni hiyo imeendelea kupanua shughuli zake katika maeneo mbalimbali nchini, ikiwamo Chunya, Mbeya, Arusha, Marerani na Lugoba mkoani Pwani, pamoja na maeneo ya ukanda wa Ziwa, ikiwamo Geita.
Sisty amesema kuongezeka kwa matumizi ya teknolojia katika sekta ya uchimbaji kunatoa fursa kwa wachimbaji kutumia mbinu za kisasa kulingana na mazingira wanayofanyia shughuli zao.
Amesema kampuni hiyo itaendelea kuongeza huduma na vifaa vya kisasa ili kukidhi mahitaji ya wachimbaji katika maeneo mbalimbali nchini.
Kwa hatua hiyo, ESEH INVESTMENTS inaendelea kujitanua katika sekta ya uchimbaji kwa kuchanganya uuzaji wa vifaa na huduma za kitaalamu, huku ikilenga kuwafikia wachimbaji wa viwango mbalimbali.

Comments
Post a Comment