Na Wellu Mtaki, Geita
MCHUNGAJI Bonifance Josephat Mwamposa, ambaye pia ni mmoja wa wachimbaji wa madini, anatarajiwa kushiriki katika Maonesho ya Teknolojia ya Madini yanayoendelea mkoani Geita, huku wachimbaji na wadau wa sekta hiyo wakihimizwa kujitokeza kwa wingi.
Mwamposa anatarajiwa kuwasili katika viwanja vya EPZA, eneo la Viwanja vya Samia Suluhu Hassan, jijini Geita, siku ya Ijumaa, Oktoba 2, 2026, akiwa ameambatana na Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wachimbaji Tanzania, John Wambura.
Akizungumza kuhusu maandalizi ya siku hiyo, Katibu wa Chama cha Wachimba Madini Mkoa wa Geita, Misana Nyabange, alisema ujio wa viongozi hao utatoa fursa kwa wachimbaji, watoa huduma na wadau wengine wa sekta ya madini kukutana, kubadilishana uzoefu na kujadili namna ya kuongeza ushiriki wa Watanzania katika kunufaika na rasilimali za madini.
Nyabange alisema siku hiyo imeandaliwa kwa lengo la kuimarisha ushirikishwaji wa Watanzania katika sekta ya madini na kutoa nafasi kwa wadau kujadili fursa na changamoto zinazowakabili katika shughuli za uchimbaji
“Ni siku ambayo tutakuwa na ugeni mkubwa. Tunawaalika wachimbaji wote, watoa huduma na wadau wote wanaohusika katika mnyororo wa thamani wa sekta ya madini kufika katika maonesho haya,” alisema.
Aidha, Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, anatarajiwa kushiriki katika maonesho hayo na kuhudhuria shughuli mbalimbali, ikiwemo semina zinazolenga kutoa elimu kwa wadau wa sekta ya madini.
Kwa mujibu wa waandaaji, uwepo wa Waziri Mavunde utatoa nafasi kwa wachimbaji na watoa huduma kuwasilisha changamoto zao, kupata ufafanuzi kuhusu masuala mbalimbali yanayohusu sekta hiyo, pamoja na kujadili fursa zinazopatikana katika shughuli za madini.
Maonesho hayo yamewakutanisha pamoja wachimbaji wadogo, wa kati na wakubwa, kampuni zinazozalisha na kusambaza vifaa vya uchimbaji, wataalamu na wadau wengine wa sekta ya madini.
Mbali na kuwakutanisha wadau hao, maonesho hayo yanalenga kuonesha matumizi ya teknolojia katika kuongeza ufanisi, usalama na tija katika shughuli za uchimbaji na uchakataji wa madini.
Waandaaji wametoa wito kwa wachimbaji na watoa huduma wote wanaohusika katika mnyororo wa thamani wa madini kujitokeza kwa wingi, wakisema maonesho hayo yanatoa fursa ya kujifunza teknolojia mpya, kujenga mitandao ya kibiashara na kupata nafasi ya kuzungumza moja kwa moja na viongozi na wataalamu wa sekta hiyo.


Comments
Post a Comment