Na MASHAKA MHANDO,Tanga
Serikali imetangaza dhamira yake thabiti ya kuleta mapinduzi ya elimu ya ujuzi na ubunifu nchini, huku ikibainisha kuwa imetenga kiasi cha Shilingi Trilioni 2.8 kwenye bajeti ya Wizara ya Elimu ili kutekeleza kwa vitendo maono ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuandaa vijana kwa soko la ajira la ndani na nje ya nchi.
Hayo yamebainishwa jana na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, wakati akizindua rasmi Maadhimisho ya Wiki ya Kitaifa ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu yanayofanyika katika viwanja vya Usagara jijini Tanga, yakishirikisha zaidi ya taasisi na vyuo vikuu 90.
Waziri Mkenda amesema mabadiliko makubwa yanayoendelea katika mitaala ikiwemo ujenzi wa shule za sekondari za amali na vyuo vya VETA kila wilaya, ni matokeo ya maelekezo ya Rais Samia ambaye tangu aingie madarakani aliweka mkazo kwenye elimu inayojenga ujuzi.
"Hiki mnachokiona kwa vijana wa Tanga Tech ni matokeo ya utekelezaji wa maono ya Rais. Hapo baadaye vizazi vijavyo vitavuna matunda ya ujuzi huu," alisema Prof. Mkenda.
Prof. Mkenda aliongeza kuwa, kwa mwaka huu, vijana watashindana katika ujuzi (Skills Competition) nchini na baadaye washindi wataenda kuiwakilisha Tanzania kwenye mashindano ya kimataifa jijini Shanghai, China.
Pia, alieleza kuwa Serikali inaendelea kutoa ufadhili wa asilimia 100 kupitia 'Samia Scholarship' kwa wanafunzi waliofanya vizuri masomo ya sayansi, hisabati, TEHAMA, na uhandisi kusoma ndani na nje ya nchi.
Katika hatua nyingine, Waziri alifurahishwa na bunifu zilizofanywa na Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) kwa kutafiti dawa ya kutibu tezi dume, utafiti ambao unakamilishwa ili dawa hiyo iweze kuzalishwa viwandani.
Pia, Prof. Mkenda alikipongeza Chuo Kikuu cha Nelson Mandela ambacho tayari kimefanya utafiti na kumaliza kutengeneza bidhaa itakayotibu magonjwa ya ngozi inayotokana na mabaki ya korosho.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Husna Sekiboko, aliitaka Wizara ya Elimu kuhakikisha bunifu hizo zinahuishwa ili zikue kibiashara, kuleta faida kwa wabunifu, na kuongeza Pato la Taifa badala ya kuishia kwenye maonesho tu.
"Tunatamani kuona uwekezaji huu uliofanywa na Serikali unakwenda kuleta uhalisia. Hatutaki tena kuona models (vielelezo), zimetosha na zibaki kwenye vyumba vya madarasa. Kwenye maonesho kama haya tulete vitu halisi vinavyotatua changamoto za Watanzania na kuvuka mipaka," alisisitiza Mhe. Sekiboko.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Fedha, Msham Mmunde, alitoa hakikisho kuwa Wizara ya Fedha haitamwangusha Rais; itatoa kiasi chote cha Shilingi Trilioni 2.8 kilichotengwa kwa ajili ya Wizara ya Elimu ili kufanikisha miradi yote bila kukwamishwa.
Naye Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Ajira na Mahusino, Dkt. Irene Munisi, alisema Serikali inatoa mikopo ya asilimia 100 kwa vijana kujifunza ujuzi ili kupata nguvu kazi itakayofikia Dira ya Taifa ya 2050 na kuhimili ushindani wa soko la ajira la viwanda duniani. Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Yonah Akwilapo, alisisitiza kuwa maonesho hayo ndiyo msingi wa maendeleo ya Taifa.
Awali, akimkaribisha mgeni rasmi, Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Profesa. Carolyne Nombo, alisema maonesho hayo yanalenga kukutanisha sekta ya umma na binafsi kubadilishana uzoefu kuelekea Dira ya 2050.
Akitanguliza salamu za mkoa, Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Balozi Dkt. Batilda Burian, alimshukuru Rais Samia kwa kuboresha elimu mkoani humo ambapo bajeti ya elimu bure imepanda kutoka Shilingi Bilioni 12 hadi Bilioni 90, huku shule mpya zikiongezeka kutoka 45 hadi 94, jambo lililoongeza ufaulu kwa kiasi kikubwa katika ngazi zote.












Comments
Post a Comment