DAR ES SALAAM, AGOSTI 14, 2026
Watanzania, kampuni, taasisi na watoa huduma wenye uwezo na sifa stahiki wamehimizwa kuchangamkia fursa mbalimbali za zabuni zilizotangazwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) kuelekea maandalizi na uendeshaji wa Mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON2027).
Akitoa taarifa hiyo leo jijini Dar es Salaam, Katibu wa Kamati ya Ndani (LOC), Neema Msitha, amesema CAF imetangaza fursa mbalimbali za zabuni zinazohusiana na maandalizi na uendeshaji wa mashindano yake, ikiwamo AFCON 2027, ambayo Tanzania itaandaa kwa kushirikiana na Kenya na Uganda.
“LOC inawahimiza Watanzania wenye uwezo, sifa na nia ya kushiriki fursa hizi kufuatilia matangazo rasmi ya zabuni hizo kupitia tovuti ya CAF ambayo ni https://www.cafonline.com/inside-caf/about-us/tenders/tenders-tab/ ili kusoma masharti ya kila zabuni na kuwasilisha maombi yao kufuatana na taratibu na muda uliowekwa na shirikisho hilo” amesisitiza Msitha.
Amesema fursa hizo zinahusisha maeneo mbalimbali, yakiwamo michezo, biashara, huduma za kitaalamu, teknolojia, masoko, usafirishaji na malazi, pamoja na huduma nyingine zitakazohitajika kulingana na matakwa ya kila zabuni.
“Tunawajulisha Watanzania, taasisi, kampuni na wadau wenye uwezo na sifa stahiki kuwa CAF imetangaza fursa mbalimbali za zabuni zinazohusiana na maandalizi na uendeshaji wa mashindano yake, ikiwamo AFCON 2027,” amesema Msitha.
Kwa mujibu wa Msitha, fursa hizo ni muhimu kwa kampuni na watoa huduma wa ndani kupata nafasi ya kushiriki katika shughuli mbalimbali zinazohusiana na maandalizi na uendeshaji wa AFCON 2027.
Akihitimisha taarifa hiyo, Msitha amesema Tanzania iko tayari kwa ajili ya mashindano hayo na kuwataka Watanzania kuchangamkia fursa zinazojitokeza.



Comments
Post a Comment