KAMPALA, Uganda
Serikali ya Uganda imepanga kuanza kuhamisha kwa awamu wizara, idara na taasisi zake kutoka Kampala kwenda Nakasongola, katika mpango wa muda mrefu ambao unaweza kuendelea hadi mwaka 2040.
Mpango huo umetangazwa na Waziri wa Nchi wa Maendeleo ya Miji, Margaret Muhanga, mbele ya Kamati ya Ardhi na Nyumba ya Bunge la Uganda. Muhanga amesema Rais Yoweri Museveni anaunga mkono mpango huo, ambao Serikali inautazama kama sehemu ya utekelezaji wa maono ya maendeleo ya Uganda kuelekea mwaka 2040.
KAMPALA YAWA CHANGAMOTO
Serikali imesema msongamano mkubwa wa magari na changamoto za upangaji wa mji zimefanya Kampala kuwa na mazingira magumu kwa watu kuishi na kufanya kazi.
Muhanga amesema Uganda inapoteza takribani dola bilioni 1.6 kwa mwaka kutokana na foleni za magari, huku baadhi ya wakazi wakilazimika kuamka saa 10 alfajiri (4:00 asubuhi) ili waweze kufika kazini saa 2 asubuhi (8:00).
“Kampala haiwezi kuishiwa, haiwezi kubadilishwa, haiwezi kuendelezwa kwa hali ilivyo, na lazima tuondoke,” alisema Muhanga.
KWA NINI NAKASONGOLA?
Kwa mujibu wa Serikali, Nakasongola imeonekana kuwa na mazingira bora kwa kujenga kituo kipya cha utawala kwa sababu ya nafasi yake ya kijiografia, idadi ndogo ya watu na upatikanaji mkubwa wa ardhi.
Muhanga amesema Serikali haikuchagua miji kama Mbarara, Fort Portal na Gulu, kwa sababu nayo tayari inakabiliwa na baadhi ya changamoto za upangaji wa miji zinazofanana na Kampala.
Badala yake, Nakasongola inaonekana kutoa fursa ya kujenga mji uliopangwa tangu mwanzo, ukiwa na miundombinu ya barabara, ofisi za Serikali, makazi na huduma nyingine bila kurithi matatizo yaliyopo katika miji mikubwa.
SI MPANGO WA SIKU MOJA
Serikali inasema uhamishaji huo hautafanyika kwa mara moja. Baadhi ya wizara, idara na taasisi zinaweza kuanza kuhamishwa hatua kwa hatua, huku mchakato mzima ukiweza kuendelea hadi 2040.
Muhanga amesema mpango huo unahusishwa na Vision 2040, hivyo Serikali inalenga kuanza taratibu badala ya kuhamisha taasisi zote kwa wakati mmoja.
Mwenyekiti wa Kamati ya Ardhi na Nyumba ya Bunge, Edson Rugumayo, ameunga mkono wazo hilo na kuitaka Serikali kutoa maelezo ya hatua zinazochukuliwa ili kutekeleza mpango huo, akisema wazo la kuondoka Kampala limejadiliwa kwa muda mrefu.
KAMPALA HAITAACHWA
Licha ya mpango huo, Serikali imesisitiza kwamba Kampala itaendelea kuwa muhimu, hasa kama kitovu cha biashara na shughuli za kiuchumi.
Hata hivyo, baadhi ya wamiliki wa majengo ya biashara na ofisi Kampala wana wasiwasi kwamba kuondoka kwa taasisi za Serikali kunaweza kupunguza mahitaji ya majengo yao.
Muhanga amepuuzilia mbali hofu hizo, akisema Kampala itaendelea kuwepo na kwamba uhamishaji wa shughuli za Serikali hautamaanisha mwisho wa umuhimu wa jiji hilo.
WAZO LILIKUWEPO KWA MUDA
Wazo la kupunguza mkusanyiko wa shughuli za Serikali Kampala si jipya. Bunge la Uganda liliwahi kujadili mapendekezo ya kuhamisha baadhi ya shughuli za Serikali kutoka Kampala ili kupunguza msongamano na kuipa Kampala nafasi zaidi kama kitovu cha uchumi.
Mpango wa sasa wa Nakasongola, hata hivyo, unaonekana kuwa hatua mpya kwa sababu Serikali sasa inazungumzia utekelezaji wa awamu kwa awamu hadi 2040, badala ya kubaki kwenye mjadala pekee.

Comments
Post a Comment