NA: MWANDISHI WETU, TANGA
Katika kuhakikisha wafanyabiashara wanakuwa na uelewa wa kutosha kuhusiana na mabadiliko ya sheria za kodi kwa mwaka 2026/2027, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) mkoa wa Tanga, imetoa mafunzo kwa wafanyabiashara mkoani humo.
Mafunzo hayo yametolewa Agosti 12, 2026, katika Ukumbi wa YDCP Jijini Tanga. Katika mafunzo hayo, wafanyabiashara wamejengewa uwezo juu ya mabadiliko mbalimbali ya sheria za kodi yaliyofanyika ili kuiwezesha TRA kutekeleza majukumu waliyopangiwa na serikali kuu.
Akifungua mafunzo hayo, Meneja wa TRA mkoa wa Tanga, CPA. Castro John, amesema sheria zaidi ya 15 za kodi zimefanyiwa mabadiliko, hivyo wanalo jukumu la kutoa elimu kwa wafanyabiashara.
"Niwashukuru wafanyabiashara wa Tanga kwa kujitokeza kupata elimu hii muhimu kwani wafanyabiashara wanapokuwa na uelewa wa mabadiliko haya, basi utekelezaji wa ulipaji kodi utakuwa mwepesi," amesema CPA John.
Maofisa mbalimbali kutoka TRA Makao Makuu waliwaelimisha wafanyabiashara hao mabadiliko ya sheria mbalimbali za kodi ambazo utekelezaji wake una mchango wa moja kwa moja katika kufanikisha mipango mbalimbali ya kodi.
Naye, Afisa Elimu ya Mlipakodi na Mawasiliano kutoka TRA Makao Makuu, Hamisi Sanze, alitoa mada juu ya Sheria ya Kodi ya Mapato, amesema, serikali imedhamiria kuinua sekta ya madini ili iendelee kuchangia pato la taifa.
Amesema, katika sura ya 332, serikali imetoa msamaha wa kodi ya mapato kwa mmiliki wa leseni ya uchimbaji wa madini (Mining licence) au leseni maalum ya uchimbaji madini.
Pia amesema, katika kuendelea kuweka mazingira wezeshi kwa sekta hiyo, Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) Sura 148 imeeleza kuwa, bidhaa na huduma zinazoangizwa au kununuliwa na mwenye leseni ya madini au leseni maalum ya madini zitapata msamaha wa kodi.
Aidha, msamaha huo utatumika kwa bidhaa na huduma zinazotumika katika ujenzi wa mradi wa madini na utakoma uzalishaji wa madini utakapoanza.
Katika hatua nyingine, Sanze amesema, kwa mujibu wa Sheria ya Ushuru wa Bidhaa, Sura 147; inafafanua kuwa, watoa huduma za mitandao wasio wakazi, wanatakiwa kujisajili, kupata TIN, kutoza, kuwasilisha ritani na kulipa ushuru wa bidhaa kwa huduma zinazotolewa.
Kwa upande wake, Afisa Mkuu Msimamizi wa Kodi, Salim Bakari, amesema kwa mujibu wa Sheria za Usimamizi wa Kodi, Sura ya 438 ni kwamba, mtu anayepaswa kulipa kodi kutokana na ajira, biashara na uwekezaji anatakiwa kuomba Namba ya Utambulisho wa Mlipakodi (TIN) ndani ya siku 15 tangu aanze shughuli hizo.
Aidha, kifungu cha 73(4) kinaeleza, Kamishna Mkuu wa TRA, amepewa mamlaka ya kuuza bidhaa zilizokamatwa ambazo zinaharibika haraka kwa njia ya mnada au mauzo ya moja kwa moja
Sambamba na hilo, amesema kifungu cha 95, kinatoa onyo kwa mtu anayehusika kurekodi taarifa za uongo au zisizo sahihi kwenye vitabu vya hesabu, rejesta au mifumo, kwani kwa kufanya hivyo, atapaswa kulipa adhabu mara mbili ya kodi aliyokwepa au aliyopunguza kulipa.
Halikadhalika, Bakari, amewakumbusha wafanyabiashara wa Jiji la Tanga kuwa, serikali imetoa msamaha wa kodi kwa kipindi cha mwaka mmoja kwa mfanyabiashara anayeanza biashara kwa mtaji usiozidi milioni 200.
Pia, amewakumbusha, malipo ya ada za shule, utalii, tozo, bidhaa, huduma, ununuzi wa magari, mashamba, viwanja, yafanyike kieletroniki ili kuongeza ufanisi wa ukusanyaji mapato ya serikali.
Akihitimisha mafunzo hayo, Meneja Msaidizi Ukaguzi na Ufuatiliaji TRA mkoa wa Tanga, Daniel Ramadhani, amewasisitiza wafanyabiashara kulipa kodi kwa uaminifu mkubwa kwani ndizo zinazowezesha serikali kutoa huduma nzuri kama elimu, afya, maji, miundombinu, umeme kwa wananchi wake.
Pia, ametoa wito kwa wafanyabiashara na walipakodi kwa ujumla, kuwasilisha changamoto zao ili zifanyiwe kazi kwani wapo kwa ajili ya kuwahudumia.
Ikumbukwe kuwa, bajeti ya mwaka 2026/2027, TRA inapaswa kukusanya shilingi trilioni 41.80 ambayo ni sawa na asilimia 67 ya bajeti nzima ya shilingi trilioni 62.33. Bajeti hii ndiyo bajeti ya kwanza kuelekea utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050.








Comments
Post a Comment