TAASISI YA SANJEEV MANSOTRA NA MBUNGE MAVUNDE WAKABIDHI MADARASA 10 NA MAABARA 3 ZA SAYANSI JIJINI DODOMA
Taasisi ya Sanjeev Mansotra Foundation kwa ushirikiano na Mbunge wa Jimbo la Mtumba Mh. Anthony Mavunde wamekabidhi madarasa 10 na maabara 3 za sayansi zenye jumla ya thamani ya Tsh 444,700,000 kwa shule ya Sekondari Anthony Mavunde-Mkoyo,Hombolo na Shule ya Msingi Makutupora.
Akizungumza katika hafla hiyo,Mbunge Mavunde amewashukuru wananchi wa Mkoyo kwa kumuunga mkono wakati anaanzisha ujenzi wa shule hiyo ili kuwanusuru watoto waliokuwa wakitembea kilomita 18 kufuata Shule.
Aidha, Mavunde ameishukuru serikali chini ya uongozi wa Mh. Rais Dkt. Samia S. Hassan kwa kuunga mkono juhudi hizo na kuchangia ujenzi wa madarasa ambayo inawafanya wanafunzi wasome katika mazingira ya utulivu.
Aidha,Mbunge Mavunde ameishukuru Taasisi ya Sanjeev Mansotra kwa ujenzi wa madarasa na maabara ambazo zitasaidia wanafunzi kuwa na mazingira mazuri ya ufundishwaji na kupunguza msongamano wa wanafunzi hasa kwa Shule ya Msingi Makutupora.
Akitoa salamu zake,Mwakilishi wa Taasisi ya Sanjeev Mansotra Ndg. Darchite Kantelal amepongeza hatua kubwa ya kuwajali wananchi ambayo Mbunge Mavunde ameionesha kwa vitendo na kuahidi kwamba Taasisi hiyo ipo tayari kuendelea kushirikiana na Jimbo la Mtumba kwa ajili ya kuwaletea wananchi maendeleo na hasa utatuzi wa changamoto za msingi zinazowakabili wananchi.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mh. Jabir Shekimweri ameitaka jamii kuzingatia umuhimu wa elimu na kuhakikisha watoto wanapewa nafasi hii muhimu ya kujengewa maarifa na hasa kwa kuwa serikali imeweka mazingira wezeshi ya ufundishaji na miundombinu rafiki.
Wakitoa salamu zao Mstahiki Meya wa Jiji la Dodoma Mh.Almon Chaula na Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Dodoma Mjini Cde Charles Mamba,wamempongeza Mbunge Mavunde kwa kuwa mstari wa mbele wa utatuzi wa changamoto za wananchi wa Jimbo la Mtumba na kuahidi ushirikiano wa kutosha kwa Mh. Mavunde katika kutimiza majukumu yake.











Comments
Post a Comment