Mhe. Senyamule ametoa kauli hiyo leo, Agosti 11, 2026, baada ya kutembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa uwanja huo, ambapo pia amepata fursa ya kuzungumza na kusikiliza changamoto za wafanyakazi wanaoshiriki katika utekelezaji wa mradi huo.
Amesema uwanja huo ni miongoni mwa miradi mikubwa na ya kimkakati inayotekelezwa na Serikali, ukiwa na umuhimu mkubwa kwa Mkoa wa Dodoma na Taifa kwa ujumla kutokana na uwezo wake wa kuchochea maendeleo ya michezo, ajira na shughuli mbalimbali za kiuchumi.
“Mradi huu ni wa kimkakati kwa Mkoa wa Dodoma na kwa nchi yetu kwa ujumla. Ndiyo maana tumeona kuna sababu ya kuja kutembelea na kujua ujenzi unavyoendelea, lakini pia kuwasikiliza ninyi mnaoshiriki katika kuujenga,” amesema Mhe. Senyamule.
Ameishukuru Serikali inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutoa fedha na kusimamia utekelezaji wa mradi huo, akisema uwekezaji huo unalenga kuwapatia Watanzania mazingira bora ya kushiriki katika michezo, huku ukifungua fursa za ajira na biashara.
Kwa mujibu wa Mkuu huyo wa Mkoa, uwanja huo unajengwa kwa kuzingatia viwango vya kimataifa, ikiwemo mahitaji ya FIFA na mashindano makubwa ya soka barani Afrika.
Amesema kukamilika kwa uwanja huo kutaongeza uwezo wa Dodoma kuwa mwenyeji wa mashindano makubwa ya michezo, ikiwemo kupokea timu mbalimbali kwa ajili ya mashindano na mazoezi, hatua ambayo itaongeza shughuli za kiuchumi katika Mkoa wa Dodoma.
Mhe. Senyamule amesema mradi huo tayari umefungua ajira kwa vijana zaidi ya 200, huku idadi hiyo ikibadilika kulingana na mahitaji ya kazi katika hatua mbalimbali za ujenzi.
Amesema kinachofurahisha zaidi ni kuona vijana kutoka maeneo mbalimbali ya Tanzania wakifika Dodoma na kutumia fursa zinazotokana na mradi huo kujiajiri na kuongeza ujuzi.
“Hii ndiyo Tanzania. Fursa ni ya Watanzania wote. Vijana wametoka kusini, kaskazini, mashariki na magharibi na wamekuja Dodoma kushiriki katika ujenzi huu na kupata ajira. Hii ni fursa iliyotengenezwa kwa ajili ya vijana wote,” amesema.
Aidha, amewataka wafanyakazi wanaoshiriki katika ujenzi huo kuwa walinzi wa kwanza wa mradi kwa kutunza vifaa, miundombinu na rasilimali nyingine zinazowekwa na Serikali, pamoja na kutoa taarifa kwa viongozi pale wanapobaini viashiria vya wizi, uharibifu au uzembe.
Amesema kila mfanyakazi ana wajibu wa kuhakikisha mradi unatekelezwa kwa ubora uliokusudiwa, kwa kuwa fedha zinazotumika ni rasilimali za Watanzania.
“Macho yenu yanaona na masikio yenu yanasikia. Kazi yenu kubwa ni kulinda rasilimali za nchi ambazo zimewekezwa hapa. Kama wewe ni engineer na unaona jambo ambalo halijaenda sawa, sema. Huu ni wajibu wetu wa kulinda nchi yetu,” amesisitiza.
Nao baadhi ya wafanyakazi katika uwanja huo akiwemo Emmanuel Mang'ombe amesema ujenzi unaendelea vizuri na hatua kubwa imekwishafikiwa katika maeneo mbalimbali ya mradi ambapo Amesema baadhi ya kazi zimefikia hatua za juu za utekelezaji, huku mwenendo wa ujenzi ukiendelea kuonyesha matarajio ya kufikiwa kwa hatua muhimu za mradi katika miezi ijayo.
Mang'ombe amesema mradi huo umeendelea kuwa na manufaa kwa jamii inayouzunguka, hususan kwa kutoa ajira kwa vijana na kuongeza fursa za kiuchumi kwa wafanyabiashara wadogo wanaotoa huduma kwa wafanyakazi, wakiwemo mama ntilie na wauzaji wa vyakula.
Amesema wafanyakazi wameendelea kuthamini uwekezaji huo kutokana na fursa za ajira, malipo na uwezekano wa kuongeza uzoefu katika utekelezaji wa mradi mkubwa wa miundombinu ya michezo.
Kwa upande wake, Upendo Yusuf Charles, Site Engineer, amesema ujenzi wa uwanja huo umekuwa fursa muhimu kwa vijana kupata ajira na kuongeza ujuzi wa kitaalamu kupitia ushiriki wao katika mradi wenye viwango vya kimataifa.
Amesema mradi huo umewapa nafasi wataalamu na wafanyakazi wenye viwango tofauti vya elimu na utaalamu kushiriki katika utekelezaji wake, huku vijana wakipata fursa ya kujifunza na kujenga uzoefu unaoweza kuwasaidia katika miradi mingine mikubwa.
“Sio kila siku tunapata nafasi ya kujenga viwanja vya kiwango hiki. Kupata nafasi ya kushiriki katika mradi kama huu ni fursa kubwa kwetu vijana, kwa sababu tunapata ajira lakini pia tunaongeza ujuzi na uzoefu,” amesema.
Mhe. Senyamule amewapongeza vijana wanaoshiriki katika ujenzi huo, pamoja na Wizara, wataalamu na mkandarasi kwa kazi inayoendelea, huku akisisitiza umuhimu wa kuhakikisha mradi unakamilika kwa wakati, ubora na viwango vilivyokusudiwa.
Amesema kukamilika kwa Uwanja wa Mpira wa Miguu wa Dodoma kutakuwa hatua muhimu katika kuimarisha sekta ya michezo, kuongeza fursa za ajira na kuchochea shughuli za kiuchumi, si kwa Dodoma pekee bali kwa Watanzania kwa ujumla.





Comments
Post a Comment