Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, ametoa muda wa siku saba kwa wananchi wa Toangoma, Wilaya ya Temeke, wanaodaiwa kuvamia eneo linalomilikiwa na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), ili kutafakari na kutafuta ufumbuzi wa haraka ili pande zote ziweze kufikia hatua ya kupata haki kutokana na mgogoro huo.
Hayo ameyabainisha mapema leo, Agosti 19, 2026, katika mkutano na wananchi wa eneo hilo mara baada ya kusikiliza maelezo kutoka kwa wananchi, uongozi wa NSSF na Ofisi ya Kamishna wa Ardhi. Katika mkutano huo, ilibainika kuwa eneo hilo ni mali ya NSSF, hivyo Mkuu wa Mkoa amesisitiza umuhimu wa kutafuta suluhisho la kibinadamu ili kutatua mgogoro huwo.
Aidha Chalamila amewataka wananchi hao kuwa waungwana kwa kutambua chanzo cha mgogoro huwo n kutumia njia za kuzungumza badala ya kufikishana katika mamlaka za kisheria inaweza kuumiza baashi ya wananchi kutokana na uhalali wa viwanja hivyo.
Kwa upande wa Kamishna Msaidizi wa Ardhi Mkoa wa Dar es Salaam, Rehema Mwinuka, alithibitisha mbele ya mkutano kuwa eneo hilo limesajiliwa rasmi kwa jina la NSSF. Kwa upande wake, Meneja wa Mali wa NSSF alifafanua kuwa uamuzi wa kuuza ardhi hiyo ulikuja baada ya kubaini kuwepo kwa ujenzi holela na uvamizi, hivyo wakaona ni vyema kuwapa fursa wananchi waliopo katika eneo hilo kununua viwanja badala ya kuwavunjia nyumba zao.
Aidha, wananchi hao wameuomba uongozi wa NSSF kuwapunguzia bei ya viwanja hivyo, ambapo kwa sasa wanatakiwa kulipa shilingi 15,000 kwa mita ya mraba katika eneo la Malela na shilingi 25,000 kwa mita ya mraba katika eneo la Mwapemba. Wananchi hao wamesema viwango hivyo ni vikubwa ukilinganisha na uwezo wao wa kiuchumi, hivyo wamependekeza bei ishushwe hadi shilingi 5,000 kwa mita ya mraba.
Kwa mujibu wa taarifa za wananchi hao, walisema walifanikiwa kununua viwanja hivyo kupitia viongozi wa mitaa yao bila kufahamu kuwa ardhi hiyo ilikuwa inamilikiwa na NSSF, jambo ambalo limetajwa kuwa miongoni mwa chanzo cha mgogoro huo uliodumu kwa muda mrefu.
Hata hivyo, wananchi hao wameiomba Serikali kuharakisha mchakato wa kutafuta suluhisho ili kusaidia baadhi ya familia ambazo zimekosa makazi kufuatia kubomolewa kwa baadhi ya maeneo yaliyokuwa na mgogoro.
Miongoni mwa mambo yanayotarajiwa kujadiliwa katika kipindi hicho cha siku saba ni uwezekano wa kupatikana kwa makubaliano kuhusu bei ya viwanja, namna ya kuwatambua wananchi waliokuwa tayari wamejenga katika eneo hilo pamoja na utaratibu wa kuwawezesha kupata hati halali za umiliki. Hatua hiyo inalenga kuhakikisha kuwa suluhisho litakalopatikana halitakuwa la muda mfupi pekee, bali litasaidia kumaliza mgogoro huo kwa kuzingatia sheria na maslahi ya pande zote.
Kwa mujibu wa taarifa ya Mkuu wa Mkoa Albert Chalamila, mkutano ujao kati yake na wananchi hao unatarajiwa kutoa taswira mpya kuhusu hatua zilizofikiwa katika kutatua mgogoro huo. Mkutano huo pia unatarajiwa kuangalia utekelezaji wa makubaliano yatakayofikiwa ndani ya siku saba, hatua ambayo inaweza kuwa mwanzo wa kuhitimisha rasmi mgogoro huo wa muda mrefu.









Comments
Post a Comment