WATANZANIA 669 waliopo Afrika Kusini wanatarajiwa kurejea nchini kwa hiari yao kwa msaada wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kufuatia maelekezo ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuwawezesha kurejea nyumbani na kuungana na familia zao.
Balozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini, James Bwana, ameyasema hayo leo kuwa utekelezaji wa mpango huo utaanza na kundi la kwanza la Watanzania 241 kutoka Durban, Jimbo la KwaZulu-Natal, watakaorejea nchini Agosti 26, 2026 kwa ndege ya Air Tanzania.
Kwa mujibu wa Balozi Bwana, Watanzania hao watafanyiwa uhakiki Agosti 25 na 26 kwa kushirikisha Ubalozi wa Tanzania na mamlaka za Afrika Kusini, kabla ya kuanza safari ya kurejea nchini.
Amesema mpango huo umeanza baada ya Watanzania hao kuomba kwa hiari yao msaada wa Serikali ili waweze kurejea Tanzania, baada ya kuishi Afrika Kusini kwa muda mrefu.
“Mheshimiwa Rais amewakaribisha tena nyumbani na amenielekeza kama Balozi wake hapa Afrika Kusini kuhakikisha Watanzania walio tayari kurejea kwa hiari yao wanawezeshwa kufanya hivyo,” amesema Balozi Bwana.
Balozi Bwana amesema baada ya kundi la kwanza kutoka Durban, takribani Watanzania 300 kutoka Cape Town wanatarajiwa kurejea Tanzania katika wiki ya kwanza ya Septemba.
Amesema tarehe rasmi ya safari hiyo itatangazwa na Ubalozi mara maandalizi yatakapokamilika.
Aidha, amesema kundi la mwisho litakalokamilisha idadi ya Watanzania 669 litaondoka kutoka Johannesburg, Jimbo la Gauteng, kwa tarehe itakayotangazwa baadaye.
Balozi Bwana amesema Serikali imeandaa usafiri wa kuwawezesha Watanzania hao kurejea nchini, huku akieleza kuwa zoezi hilo linatekelezwa kwa ushirikiano kati ya Ubalozi wa Tanzania na mamlaka za Afrika Kusini.
Amesema lengo ni kuhakikisha Watanzania wanaorejea wanakamilisha taratibu zote muhimu na kufika salama nchini kwa ajili ya kuungana na ndugu, jamaa na marafiki zao waliowaacha kwa miaka kadhaa.
Kwa hatua hiyo, Watanzania hao watapata fursa ya kurejea nchini na kuendelea kushiriki katika shughuli mbalimbali za kijamii na kiuchumi pamoja na ujenzi wa taifa.
Balozi Bwana amesema msaada huo umetolewa na Rais Samia baada ya Watanzania hao wenyewe kuomba kuwezeshwa kurejea nyumbani, akisisitiza kuwa Serikali imepokea ombi hilo kwa nia ya kuwawezesha wananchi wake kurejea katika nchi yao.
“Tunawakaribisha nyumbani ili waungane na ndugu, jamaa na marafiki zao na kuendelea na shughuli za ujenzi wa taifa,” amesema.
Safari hiyo inatarajiwa kufanyika Jumatano, Agosti 26, 2026, kwa ndege ya Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) kutoka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa King Shaka, Durban.


Comments
Post a Comment