Na Mwandishi Wetu, Katavi
SERIKALI imekabidhi pampu 52 za umwagiliaji zenye thamani ya zaidi ya Sh500 milioni kwa vikundi 46 vya wakulima mkoani Katavi, hatua inayolenga kuongeza tija katika kilimo, kupanua eneo linalolimwa na kuimarisha usalama wa chakula.
Pampu hizo zimekabidhiwa kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji (NIRC) katika hafla iliyofanyika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Katavi, ikiwa ni sehemu ya awamu ya kwanza ya mpango wa Serikali wa kuimarisha matumizi ya teknolojia ya umwagiliaji katika kilimo.
Mradi huo unatarajiwa kuongeza eneo la umwagiliaji kwa takribani ekari 2,080, huku ukitoa fursa kwa wakulima kuongeza uzalishaji wa mazao mbalimbali na kuboresha kipato cha kaya.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Mkuu wa Wilaya ya Tanganyika, Onesmo Buswelu, aliwataka wanufaika kutumia pampu hizo kwa malengo yaliyokusudiwa badala ya kuzigeuza kwa shughuli nyingine zisizohusiana na kilimo.
Buswelu alitoa tahadhari kwa baadhi ya wakulima dhidi ya kutumia vifaa hivyo katika shughuli kama kufyatua matofali, akisisitiza kuwa Serikali imewekeza katika pampu hizo ili kuongeza uzalishaji wa chakula na kipato cha wakulima.
Alisema pia wakulima wanapaswa kuendesha kilimo kinachozingatia uhifadhi wa mazingira, ikiwemo kuepuka kuchepusha au kuziba mito na kuharibu vyanzo vya maji.
Pampu maalumu kwa maji yanayotiririka
Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji, Raymond Mndolwa, alisema pampu hizo zimetengenezwa mahsusi kwa ajili ya maeneo yenye maji yanayotiririka na hazilengi matumizi ya visima.
Alisema katika hatua ya kulinda mazingira na kuzuia wakulima kulima pembezoni mwa vyanzo vya maji, pampu hizo zimewekewa mipira yenye urefu wa zaidi ya mita 60, inayowezesha maji kuvutwa kutoka kwenye mito, mifereji au mabwawa bila kulazimisha wakulima kwenda karibu na vyanzo vya maji.
Mndolwa aliwataka wanufaika kuhakikisha pampu hizo zinatumika kwa ajili ya kilimo pekee ili ziweze kutoa matokeo yaliyokusudiwa na Serikali.
Pampu moja kumwagilia hadi ekari 40 kwa siku
Akitoa taarifa kuhusu pampu hizo, Mhandisi wa Umwagiliaji Mkoa wa Katavi, Samson Bai, alisema pampu hizo zitasambazwa katika halmashauri zote tano za mkoa huo.
Alisema kila pampu ina uwezo wa kusukuma kati ya mita za ujazo 80 hadi 100 za maji kwa saa, huku pampu moja ikiwa na uwezo wa kumwagilia hadi ekari 40 kwa siku, kutegemea mazingira ya eneo na mfumo wa umwagiliaji unaotumika.
Aliongeza kuwa pampu hizo zimewekewa magurudumu, jambo linalorahisisha kuzihamisha kutoka eneo moja la kilimo kwenda jingine kulingana na mahitaji ya wakulima.
Wakulima waondokana na gharama za majenereta
Wakulima walionufaika na mpango huo wameeleza kuwa pampu hizo zitawasaidia kuongeza uzalishaji huku zikiwaondolea changamoto walizokuwa wakikabiliana nazo kutokana na matumizi ya majenereta ya zamani.
Mkulima Tausi Masudi alisema pampu hizo zitapunguza adha ya kutumia majenereta yaliyokuwa yakikwama mara kwa mara na kusababisha usumbufu katika shughuli za umwagiliaji, ikiwemo kuharibika kwa mipira.
Naye mkulima Chausiku Omary alimshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwawezesha kupata vifaa hivyo, akisema vitawasaidia kulima mazao mbalimbali, yakiwemo mboga mboga na mahindi.
Alisema ongezeko la uzalishaji litasaidia wakulima kuongeza kipato, kuboresha maisha ya familia zao na kuwawezesha kumudu gharama za elimu ya watoto.
Katavi ina hekta zaidi ya 124,000 za umwagiliaji
Mkoa wa Katavi una jumla ya hekta 124,761 zinazofaa kwa kilimo cha umwagiliaji.
Kati ya eneo hilo, takribani hekta 110,672 zinaendelezwa kupitia skimu 29 za umwagiliaji, zinazowezesha uzalishaji wa mazao mbalimbali, ikiwemo mpunga, mahindi, maharage na mboga mboga.
Kwa hatua hiyo, Serikali inalenga kutumia teknolojia ya umwagiliaji kuongeza tija, kupunguza utegemezi wa mvua, kuongeza uzalishaji wa chakula na kuwawezesha wakulima kuzalisha kwa uhakika zaidi mwaka mzima.
























Comments
Post a Comment