Kuelekea fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027, washiriki wa fani ya upishi katika Mashindano ya Kitaifa ya Ujuzi WorldSkills Tanzania 2026 wametakiwa kujiandaa kuwa mabalozi wa utalii na ukarimu wa Tanzania kupitia umahiri wao wa kupika.
Wito huo umetolewa leo Agosti 22,2026 na Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi, Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET), Bi. Bernadetta Ndunguru, alipotembelea mashindano yanayoendelea katika viwanja vya Shule ya Sekondari Usagara, jijini Tanga.
Ndunguru amesema washiriki hao tayari wameonesha kiwango cha juu cha taaluma na wanapaswa kujiona kama wapishi wakubwa watakaokuwa sehemu ya kuipokea Afrika wakati Tanzania itakapokuwa mwenyeji wa AFCON 2027.
Kwa mujibu wa Ndunguru, ubora wa huduma za chakula na ukarimu vinatarajiwa kuwa sehemu muhimu ya taswira ya Tanzania mbele ya maelfu ya wageni kutoka mataifa mbalimbali ya Afrika.
"Niwahimize vijana muendelee kuboresha ujuzi wenu na kutumia fursa ya WorldSkills Tanzania kama daraja la kujenga taaluma, ajira na kuitangaza Tanzania kupitia huduma zenye ubora wa kimataifa,"amesema.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Uthibiti Ubora wa NACTVET Dkt. Jofrey Oleke, amewapongeza washiriki wa fani ya ushonaji na ubunifu wa mitindo kwa umahiri waliouonesha kupitia kazi zao za kibunifu.
Amesema kila kitu katika hatua hiyo ni fursa hivyo vijana wanapaswa kuhakikisha wanatumia bunifu hizo kuendelea kufanya bunifu zenye manufaa kwao na kwa taifa kwa ujumla.
"Niwapongeza kwa hatua kubwa ya ubunifu huu mliyooneshwa katika haya mashindano umahili wao wa kubuni mavazi ni mkubwa sana hivyo niwakaribishe wananchi kuanza kuwatumia wabunifu hawa katika kazi zenu,"amesema.









Comments
Post a Comment