Wazee wa Kabila la Wazanaki wamesema kuwaka kwa mwanga mkali na tulivu kwa Mwenge wa Mwitongo mara baada ya kuwashwa ni ishara ya mwaka wenye baraka, amani na mafanikio kwa Taifa la Tanzania.
Wakizungumza katika hafla ya kuwashwa kwa Mwenge huo nyumbani kwa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Mwitongo, Agosti 2, 2026, wazee hao wamesema kwa mujibu wa mila na desturi za Wazanaki, Mwenge huo hubeba ujumbe maalumu kuhusu mwenendo wa taifa kila unapowashwa.
"Kwa miaka mingi tumekuwa tukishuhudia kuwa endapo kuna dalili zisizo njema kwa taifa, Mwenge huu huonesha ishara zake mara baada ya kuwashwa. Leo tumeshuhudia ukiwaka vizuri sana bila hitilafu yoyote. Hii ni ishara njema na tunaliombea taifa letu liendelee kuwa na amani, umoja na maendeleo," wamesema baadhi ya wazee walioshuhudia tukio hilo.
Wazee hao waliipongeza Serikali kwa kuendelea kuenzi urithi wa kihistoria wa Mwitongo, wakieleza kuwa utamaduni huo unaendelea kuimarisha historia ya Taifa na kumuenzi Baba wa Taifa.
Katika hafla hiyo, Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Ndugu Wazo Michael Mwang'onda, aliwasha Mwenge wa Mwitongo kwa kutumia Mwenge wa Uhuru, ikiwa ni sehemu ya shughuli za kitaifa za Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2026.
Mwenge wa Uhuru ulipowasili Mwitongo ulipokelewa na familia ya Baba wa Taifa ikiongozwa na Chifu wa Kabila la Wazanaki, Japhet Wanzagi, ambaye pia ni msimamizi wa familia ya Baba wa Taifa.
Tukio hilo lilihudhuriwa na Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi, viongozi wa Serikali, viongozi wa Wilaya ya Serengeti, wawakilishi wa vyama vya siasa na mamia ya wananchi waliojitokeza kushuhudia tukio hilo la kihistoria.








Comments
Post a Comment