Wakati Maonesho ya Kitaifa ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu yakiendelea katika viwanja vya Shule ya Sekondari Usagara jijini Tanga, mwanafunzi wa mkondo wa Amali kutoka Shule ya Sekondari Tanga Ufundi, Neema Bundara (16) ameonesha umahiri wa kuchambua na kuelezea mfumo mzima wa injini ya gari.
Akionesha umahiri huo leo Agosti 21,2026 mwanafunzi huyo wa kidato cha Tatu ametumia mfano wa injini kuonesha kazi za sehemu mbalimbali zinazounda mfumo wa injini, akieleza namna kila kifaa kinavyoshirikiana kuzalisha nguvu ya kuendesha gari.
Katika maelezo yake amesema cylinder block, pistoni na connecting rod hufanya kazi kwa pamoja kuruhusu pistoni kusogea juu na chini, hatua inayowezesha mzunguko wa mwako ndani ya injini.
"Crankshaft na camshaft huunganishwa na timing chain ili kuratibu mzunguko wa injini na kuhakikisha vali zinafunguka na kufunga kwa wakati sahihi,"ameeleza.
Aidha, akielezea mfumo wa kudhibiti uchafuzi wa mazingira, amesema catalytic converter, muffler na tail pipe husaidia kupunguza sumu na kelele za moshi kabla haujatolewa nje ya gari.
Uwezo huo unaakisi namna elimu ya Amali inavyoendelea kuwajengea vijana ujuzi wa vitendo unaoweza kuwa msingi wa ajira, ubunifu na maendeleo ya sekta ya magari nchini.

Comments
Post a Comment