KIGALI.
Taasisi ya Upelelezi nchini Rwanda (Rwanda Investigation Bureau (RIB) imemkamata Mkuu wa Mamlaka ya Chakula na Dawa nchini humo (FDA), Profesa Emile Bienvenu, pamoja na watuhumiwa wengine 17, wakiwemo maofisa 10 wa FDA.
Watu hao wanakabiliwa na tuhuma zinazohusiana na uzalishaji, usambazaji na udhibiti wa vinywaji vya kilevi visivyokidhi viwango na vinavyodaiwa kuuzwa kinyume cha sheria.
Hatua hiyo inakuja baada ya Rwanda kuendesha kampeni kubwa dhidi ya wazalishaji wa vileo wanaokiuka kanuni za usalama na afya ya umma.
Katika operesheni hiyo, zaidi ya kampuni 140 zimefungiwa, huku mamia ya bidhaa za vileo zikiondolewa sokoni na baadhi ya bidhaa kutoka nje zikizuiwa au kuwekwa chini ya masharti maalumu.
Miongoni mwa bidhaa zilizoingia kwenye hatua hizo ni baadhi ya bidhaa za vileo kutoka Uganda, zikiwemo Uganda Waragi, Bond 7, Gilbeys na V&A Sherry.
Kwa mujibu wa wachunguzi, baadhi ya maofisa wanatuhumiwa kutumia vibaya madaraka yao kwa manufaa binafsi, huku wengine wakidaiwa kuwasaidia wazalishaji ambao walikuwa wakiendesha shughuli zao katika mazingira yasiyokidhi viwango vya usafi na bila vibali vinavyohitajika.
Watuhumiwa hao wanakabiliwa na uwezekano wa hukumu za kifungo cha miaka saba hadi 10 pamoja na faini kubwa, iwapo watapatikana na hatia mahakamani.
Hatua hiyo imeongeza uzito wa kampeni ya Serikali ya Rwanda dhidi ya bidhaa za vileo zisizokidhi viwango, ambayo sasa imepanuka kutoka kuwafuatilia wazalishaji na waagizaji wa bidhaa hizo hadi kuwachunguza maofisa waliokuwa na jukumu la kuzisimamia na kuzidhibiti.
Operesheni iliyoanza kwa kulenga wazalishaji wa vileo sasa imefika kwa wale waliokuwa na jukumu la kuhakikisha sheria na viwango vinafuatwa.


Comments
Post a Comment