MBUNGE wa Jimbo la Serengeti, Mhe. Mary Daniel Surati ameambatana na Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mheshimiwa Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa, katika ziara ya kikazi wilayani Serengeti, iliyolenga kufuatilia utekelezaji wa miradi ya maendeleo, kusikiliza changamoto za wananchi na kuweka mikakati ya kuboresha huduma muhimu katika jimbo hilo.
Katika ziara hiyo, Waziri Dkt. Bashiru amekutana na kufanya kikao na viongozi mbalimbali wa Wilaya ya Serengeti, ambapo masuala mbalimbali ya maendeleo na changamoto zinazowakabili wananchi yalijadiliwa.
Ziara hiyo pia ilimfikisha Waziri katika Kata ya Matare, ambako alizindua vyumba viwili vya madarasa katika Shule ya Msingi Igina, hatua inayotarajiwa kuimarisha mazingira ya kujifunzia na kufundishia kwa wanafunzi wa shule hiyo.
Mbunge Mary amesema kushiriki kwake katika ziara hiyo ni sehemu ya kuendelea kusimamia kwa karibu masuala ya maendeleo ya wananchi wa Serengeti, akieleza kuwa uwepo wa viongozi katika maeneo ya wananchi unasaidia kupata uhalisia wa changamoto na kuchukua hatua zinazostahili.
Amesema ataendelea kushirikiana na Serikali katika kuhakikisha miradi ya maendeleo inatekelezwa kwa wakati na wananchi wanapata huduma bora zinazokidhi mahitaji yao.
“Ziara kama hizi ni muhimu katika kusikiliza changamoto za wananchi, kufuatilia utekelezaji wa miradi na kusukuma maendeleo ya Jimbo letu,” amesema Mbunge Mary.
Ameongeza kuwa ushirikiano kati ya Serikali, viongozi wa jimbo na wananchi ni nguzo muhimu katika kuharakisha maendeleo ya Serengeti na kuhakikisha fursa zinazopatikana zinawanufaisha wananchi.



Comments
Post a Comment