Mkuu wa Mkoa wa Mara, Mheshimiwa Kanali Evans Alfred Mtambi, leo tarehe 21 Agosti 2026, amewapokea na kufanya mazungumzo na ujumbe kutoka Vi Agroforestry kuhusu maandalizi ya Kongamano la 11 la Taifa la Kilimo Misitu, litakalofanyika kuanzia tarehe 19 hadi 21 Oktoba 2026 katika Kituo cha Mafunzo cha Agroforestry (ATC), Bweri, Manispaa ya Musoma.
Mazungumzo hayo yalijikita katika maandalizi ya kongamano hilo, ambalo linalenga kuhamasisha kilimo misitu kama nyenzo ya kuongeza uzalishaji, kuhifadhi mazingira, kuimarisha usalama wa chakula na kuinua uchumi wa wananchi.
Akizungumza katika kikao hicho, Mheshimiwa Kanali Mtambi amewashukuru Vi Agroforestry kwa juhudi wanazozifanya kila msimu katika kuhakikisha vijana na Watanzania kwa ujumla wanaelewa fursa zilizopo katika sekta ya kilimo.
Aidha, ametoa wito kwa wananchi wa Mkoa wa Mara, hususan vijana, kujitokeza kwa wingi kushiriki katika kongamano hilo ili kujifunza, kubadilishana uzoefu na kuibua wigo mpya wa fursa za maendeleo ya kiuchumi kupitia kilimo.
Kwa upande wake, mwakilishi wa Vi Agroforestry Khalid Nagasaki ameishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kuweka mazingira wezeshi yanayochochea maendeleo ya sekta ya kilimo na uhifadhi wa mazingira. Alisema ushirikiano huo umewezesha utekelezaji wa programu mbalimbali zinazowanufaisha wananchi na kuchangia maendeleo ya kijamii na kiuchumi nchini.
Kongamano hilo linatarajiwa kuwakutanisha wadau mbalimbali wa sekta ya kilimo, mazingira, taasisi za utafiti, sekta binafsi, vijana na washirika wa maendeleo kwa lengo la kujadili na kubadilishana uzoefu kuhusu fursa za kilimo misitu na maendeleo endelevu.



Comments
Post a Comment