MKURUGENZI Mtendaji wa Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI), Dkt. Diwani Msemo, amesema saratani ya shingo ya kizazi ndiyo inayoongoza kwa wanawake nchini Tanzania, ikiwa pia miongoni mwa saratani zinazochangia vifo kwa kiwango kikubwa.
Dkt. Msemo amesema takribani asilimia 34 ya saratani zinazowapata wanawake nchini ni saratani ya shingo ya kizazi, akisisitiza kuwa hali hiyo inapaswa kuchukuliwa kwa uzito kutokana na ukweli kwamba ugonjwa huo unaweza kuzuilika na kugundulika mapema.
Amesema saratani ya shingo ya kizazi inaweza kuzuilika kupitia chanjo, huku uchunguzi wa mara kwa mara ukisaidia kugundua mabadiliko ya awali na kutoa matibabu kabla ugonjwa haujawa mkubwa.
“Ni saratani ambayo inaweza kuzuilika kwa chanjo, inaweza kugundulika mapema kupitia uchunguzi na inapogundulika katika hatua za awali, uwezekano wa kupona huwa mkubwa sana,” amesema Dkt. Msemo.
Amesema hali hiyo inapaswa kuwa changamoto kwa jamii, kwa kuwa kuna wanawake wanaopoteza maisha kutokana na ugonjwa ambao kwa kiasi kikubwa unaweza kuzuilika kwa kuchukua hatua mapema.
Baada ya saratani ya shingo ya kizazi, Dkt. Msemo amesema saratani ya matiti nayo ni miongoni mwa saratani zinazowapata wanawake kwa kiwango kikubwa, ikikadiriwa kuchangia takribani asilimia 10 ya saratani kwa wanawake.
Aidha, amesema saratani ya utumbo mpana imeendelea kuongezeka kwa wanawake na wanaume, huku saratani ya koo la chakula ikiwa miongoni mwa saratani nyingine zinazowapata Watanzania.
Kwa upande wa wanaume, Dkt. Msemo ameitaja pia saratani ya tezi dume kuwa miongoni mwa saratani zinazohitaji wananchi kuwa na uelewa na kuchukua hatua za uchunguzi mapema.
Ametoa wito kwa wananchi kujenga utamaduni wa kupima afya mara kwa mara na kutafuta huduma za afya mapema wanapobaini dalili au mabadiliko yasiyo ya kawaida, akisisitiza kuwa ugunduzi wa mapema ni muhimu katika kuongeza nafasi ya matibabu na kupona kwa wagonjwa wa saratani.

Comments
Post a Comment