Na Mwandishi Wetu, MBEYA
SERIKALI wilayani Mbeya imepongeza uwekezaji mkubwa wa zaidi ya Shilingi Bilioni 15.5 uliofanywa katika Kiwanda cha U Fresh kilichopo Mbalizi, ikieleza kuwa mradi huo ni chachu muhimu katika kuzalisha ajira na kuchochea ukuaji wa uchumi wa viwanda mkoani humo.
Pongezi hizo zimetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Mhe. Solomon Itunda, alipoongoza Kamati ya Usalama ya Wilaya hiyo kufanya ziara ya ukaguzi wa shughuli za uzalishaji katika kiwanda hicho kilichopo mkabala na Uwanja wa Ndege wa Songwe.
Akizungumza mara baada ya Kamati hiyo kujionea shughuli mbalimbali za uzalishaji zinazoendelea, Mhe. Itunda alisema uwepo wa uwekezaji wa kiwango hicho unasaidia kukuza uzalishaji wa ndani, kuongeza thamani ya bidhaa zinazozalishwa nchini, na kutoa fursa nyingi za ajira kwa wananchi.
Mkuu huyo wa wilaya alitumia fursa hiyo kumshukuru na kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, akisema uwekezaji huo ni matunda ya mazingira wezeshi na rafiki yaliyowekwa na Serikali ya Awamu ya Sita.
"Serikali chini ya uongozi wa Rais Samia imeendelea kutoa kipaumbele kikubwa katika kukuza sekta binafsi na kuvutia uwekezaji wenye tija. Mazingira haya ndiyo yanayowavutia wawekezaji kuja kuweka mitaji yao na hatimaye kuimarisha uchumi wetu," alieleza Mhe. Itunda.
Akihitimisha ziara hiyo, Mhe. Itunda alisisitiza kuwa Kamati ya Usalama ya Wilaya haitaishia hapo, bali itaendelea kufanya ziara endelevu za ufuatiliaji na ukaguzi wa miradi na uwekezaji mbalimbali wilayani humo, ili kuhakikisha unatekelezwa kwa kuzingatia viwango vinavyotakiwa na kuwanufaisha wananchi ipasavyo.









Comments
Post a Comment