Skip to main content

@marato_tv

@marato_tv
#sauti_ya_jamii

TARI YAADHIMISHA MIAKA 10 KWA MARATHON NA MAONESHO YA TEKNOLOJIA ZA KILIMO


 Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Rosemary Senyamule, ametoa wito kwa wananchi wa Mkoa wa Dodoma na Watanzania kwa ujumla kujitokeza kwa wingi kushiriki Marathon ya TARI itakayofanyika Agosti 2, 2026, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 10 ya Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI).

Mhe. Senyamule ameyasema hayo mara baada ya kutembelea banda la TARI na kukabidhiwa jezi za marathon hiyo, ambapo alieleza kuwa mgeni rasmi katika maadhimisho hayo anatarajiwa kuwa Waziri wa Kilimo, Mhe. Daniel Chongolo. Amesema marathon hiyo inalenga kuhamasisha afya, kuunganisha wadau wa sekta ya kilimo na kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu mchango wa TARI katika utafiti na maendeleo ya kilimo nchini.

Amesema hadi sasa zaidi ya washiriki 1,000 wamekwishajisajili, huku akiwahimiza wananchi wengine kuendelea kujisajili ili kushiriki mbio hizo zitakazoanzia eneo la Nzuguni saa 2:00 asubuhi. Marathon hiyo itakuwa na mbio za kilomita 5, 10 na 21, ili kutoa nafasi kwa makundi mbalimbali ya washiriki.

Kwa mujibu wa TARI, maadhimisho ya miaka 10 tangu kuanzishwa kwake rasmi mwaka 2016 yataenda sambamba na marathon pamoja na maonesho yatakayoonesha mafanikio, teknolojia na matokeo ya tafiti zilizofanywa na taasisi hiyo katika kipindi cha miaka kumi. Maonesho hayo yatatoa fursa kwa wananchi na wadau mbalimbali wa sekta ya kilimo kujionea mchango wa TARI katika kuimarisha kilimo na kujifunza teknolojia mbalimbali zilizobuniwa na taasisi hiyo.

Maadhimisho hayo yanayobeba kauli mbiu “Utafiti kwa Usalama wa Chakula” yanatarajiwa kukutanisha wadau mbalimbali wanaoshirikiana na TARI katika shughuli za utafiti na maendeleo ya kilimo, kwa lengo la kuendelea kuimarisha usalama wa chakula na kuongeza tija katika sekta ya kilimo nchini.

Comments