DKT. JUDITH MHINA SPENDI AIPEPERUSHA BENDERA YA TANZANIA KWENYE JUKWAA LA KIMATAIFA LA UCHUMI WA BAHARI CHINA
Zhoushan, China.
Mfanyabiashara mashuhuri wa Kitanzania na Mkurugenzi wa PMM Group, Dkt. Judith Mhina Spendi, ameendelea kuipeperusha vyema bendera ya Tanzania kimataifa baada ya kushiriki mkutano wa kibiashara katika sekta meli unaowakutanisha viongozi, wawekezaji na wadau wa sekta ya bandari, uchukuzi na usafirishaji wa baharini kutoka mataifa mbalimbali, uliofanyika Shipyard Jijini Zhoushan Nchini China.
Ushiriki wa Dkt. Judith katika mkutano huo unaashiria kuongezeka kwa nafasi ya Watanzania, hususan wanawake, katika majukwaa ya kimataifa yanayojadili mustakabali wa biashara ya baharini, uchumi wa buluu na maendeleo ya sekta ya usafirishaji duniani.
Dkt. Judith ni miongoni mwa wanawake wachache nchini Tanzania waliofanikiwa kujenga na kuongoza kampuni kubwa inayotoa huduma za ugavi na usafirishaji wa mizigo kupitia bahari.
Kupitia PMM Group, kampuni hiyo imejipambanua katika huduma za usafirishaji wa mizigo katika Bahari ya Hindi, usimamizi wa bandari za nchi kavu (Dry Ports), pamoja na kutoa huduma katika sekta za madini na mazingira.
Wadau wa sekta hiyo wanaeleza kuwa ushiriki wake katika mkutano huo ni fursa muhimu ya kuitangaza Tanzania kama kitovu cha biashara na uwekezaji katika ukanda wa Afrika Mashariki, sambamba na kujenga ushirikiano mpya utakaosaidia kukuza sekta ya usafirishaji na huduma za bandari.
Mbali na mafanikio ya kibiashara, Dkt. Judith ameendelea kuwa mfano wa wanawake wa Kitanzania wanaothubutu kuwekeza katika sekta zenye ushindani mkubwa, akionyesha kuwa uongozi, ubunifu na maono vinaweza kufungua fursa za kimataifa na kuchangia maendeleo ya uchumi wa taifa.
Ushiriki wake katika mkutano huo unaendelea kuipa Tanzania sauti katika mijadala ya kimataifa kuhusu maendeleo ya uchumi wa bahari, biashara na usafirishaji wa kisasa.






Comments
Post a Comment