Familia ya Ndugu Ruhumbika Machumu Kasanje, mkazi wa Kijiji cha Chirorwe aliyekuwa anaidai fidia Kampuni ya Wakazi Mining Limited imelipwa kufuatia maelekezo ya Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Kanali Evans Alfred Mtambi aliyoyatoa katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika kijiji hicho jana tarehe 21 Julai, 2026.
Akizungumza leo tarehe 22 Julai, 2025 baada ya familia hiyo kulipwa fidia na kuhama katika eneo hilo, Mhe. Mtambi amepongeza hatua hiyo kwa kuwa inamaliza mgogoro uliodumu kwa muda mrefu na kuyaondoa maisha ya familia hiyo katika hatari za kiusalama baada ya baadhi ya watu waliokuwa wamepata ajira kwenye mgodi huo kuifanyia vurugu za kuharibu mazao ya familia hiyo baada ya mgodi huo kufungwa.
“Kulipwa kwa fidia hiyo kunatuwezesha kuufungua tena mgodi huo uendelee na shughuli zake za kawaida za uchimbaji wa madini ambapo watu zaidi ya 400 wamepata ajira na maisha yao yanategemea mgodi huo” amesema Mhe. Mtambi.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara, Mhe. Mtambi alitoa saa 24 kwa mwananchi huyo kulipwa fidia ya ardhi kupisha shughuli za uchimbaji wa madini katika eneo hilo na kuitaka kampuni hiyo kulipa fedha za usumbufu kwa familia hiyo pamoja na kodi ya miezi sita kwa ajili ya familia hiyo wakati familia hiyo inaendelea kujenga makazi ya kudumu.
Awali, familia ya Sanje ilitoa malalamiko kwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba tarehe 04 Julai, 2026 katika mkutano wa hadhara uliofanyika Suguti, Halmashauri ya Wilaya ya Musoma, kuomba kulipwa fidia kutokana na shughuli za uchimbaji kufanyika karibu na makazi yao na kuwasababishia usumbufu unaotokana na kelele na kurushiwa mawe katika makazi yao.
Akizungumza katika mkutano huo, Waziri Mkuu alimwagiza Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Mara kuisikiliza kero ya familia hiyo na kutoa mrejesho Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara na kuutaka Mkoa wa Mara kuhakikisha mgogoro huo unatafutiwa ufumbuzi wa kudumu na kusitisha shughuli zote za uchimbaji wa madini hadi mgogoro huo utakapotatuliwa.
Baada ya kupokea mrejesho kutokana kwa Afisa Madini, Kamati ya Usalama ya Mkoa imesikiliza pande zote mbili katika mgogoro huo na Mkuu wa Mkoa kuagiza familia hiyo ilipwe fidia ndani ya saa 24 ili kulinda usalama wa familia hiyo na kuhakikisha shughuli za uchimbaji madini haziathiri maisha ya wananchi.
Familia hiyo leo imelipwa shilingi milioni 40 kama fidia na shilingi milioni 3 kwa ajili ya usumbufu na kodi ya miezi sita kwa ajili ya kuihifadhi familia hiyo wakati inaendelea kutafuta makazi ya kudumu na Halmashauri ya Wilaya ya Musoma imeisaidia familia hiyo kuhama eneo hilo kwenda kwenye makazi ya muda wakati ikijipanga kupata makazi ya kudumu.
Akizungumzia suala hilo, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Musoma Ndugu Msongera Parela amesema tayari familia hiyo imeshapokea malipo ya fidia na wameishukuru Serikali kwa kufanikisha kulipwa kwa fidia hiyo ambayo ilisababisha mgogoro uliodumu kwa muda mrefu.
Ndugu Parela amesema baada ya kupokea fidia hiyo, tayari familia hiyo imeshahama katika eneo hilo na kampuni ya Wakazi Mining Limited ipo huru kuendelea na shughuli za uchimbaji wa madini katika eneo hilo bila kuathiri mtu yoyote.












Comments
Post a Comment