MBUNGE wa Tarime Vijijini, Mwita Waitara ameibana Serikali kuhakikisha fedha zinazotengwa kwa ajili ya barabara zinatumika kwa kazi hiyo pekee huku akitaka wakandarasi wanaojenga chini ya kiwango kuwajibishwa kwa kuisababishia Serikali hasara kubwa.
Waitara amesema hayo leo Mei 21, 2026 Bungeni Jijini Dodoma wakati akichangia Bajeti ya Wizara ya Ujenzi, ambapo alieleza kuwa wananchi wa Tarime, Serengeti na Mkoa wa Mara kwa ujumla wanaendelea kupata adha kubwa kutokana na ubovu wa miundombinu ya barabara.
Amesema barabara ya kilomita 87 kuelekea Mgumu Serengeti ambayo tayari imeanza kujengwa bado inakabiliwa na changamoto kubwa baada ya baadhi ya wakandarasi kuondoka eneo la mradi kutokana na ukosefu wa fedha, hali inayosababisha watalii na wananchi kupata usumbufu mkubwa wanaposafiri katika maeneo hayo muhimu ya kiuchumi na utalii.
Mbunge huyo pia ametaja barabara muhimu zinazohitaji maboresho haraka kuwa ni pamoja na Musoma–Makoko, Musoma–Bunda, Tarime–Serengeti, Mtegi–Sirari pamoja na Makutano–Mgumu Serengeti kupitia Butiama, akisema barabara hizo zina mchango mkubwa katika kukuza biashara, usafirishaji na uchumi wa wananchi wa Mkoa wa Mara.
Aidha, Mhe. Waitara amesema taarifa za Kamati zinaonyesha zaidi ya asilimia 70 ya barabara nchini ziko kwenye hali mbaya, jambo ambalo linaonyesha ukubwa wa changamoto iliyopo kwenye sekta ya miundombinu.
Katika mchango wake huo, Waitara alihoji ubora wa baadhi ya barabara zinazojengwa na kuharibika kabla hata muda wake wa matumizi kuisha, akitolea mfano barabara ya Iringa–Dodoma ambayo amesema imeanza kuharibika mapema licha ya kutotimiza muda wake wa kudumu. Amesema hali hiyo inaibua maswali makubwa kuhusu ubora wa kazi zinazofanywa na baadhi ya wakandarasi nchini.
Pia ametaja changamoto katika barabara za Mwegumbi–Maswa–Bariadi pamoja na maeneo ya Babati na Arusha, akisema baadhi ya miradi imekuwa ikisuasua huku mingine ikiharibika muda mfupi baada ya kukamilika.
“Fedha za Watanzania zinaendelea kupotea huku baadhi ya wakandarasi wakijenga barabara zisizodumu. Lazima hatua kali zichukuliwe dhidi ya wote wanaohusika,” amesema Waitara.
Mbunge huyo ameishauri Serikali kuweka mkakati maalum wa kuwawajibisha wakandarasi wanaotekeleza miradi chini ya kiwango, ikiwemo kuchukuliwa hatua za kisheria na kufilisiwa kwa wale watakaobainika kuisababishia Serikali hasara.
Pia amehoji mfumo wa mikataba inayosababisha Serikali kuendelea kubeba gharama kubwa za madeni na riba, akitaka mikataba mibovu ipitiwe upya ili kuondoa mianya ya upotevu wa fedha za umma.
Aidha, ameitaka TRA kuongeza usimamizi wa ukusanyaji kodi na kuziba mianya ya wakwepa kodi, akisema wananchi wengi wa kawaida wanaendelea kulipa kodi huku baadhi ya wafanyabiashara wakikwepa kutoa risiti na kuchangia upotevu wa mapato ya Serikali.
Waitara amesisitiza kuwa wananchi wataendelea kuiunga mkono Serikali iwapo wataona kodi wanazolipa zinarejeshwa kwenye huduma muhimu za maendeleo hususan ujenzi wa barabara na miundombinu mingine ya msingi.



Comments
Post a Comment