MBUNGE wa Viti Maalum Mkoa wa Mara, Agnes Marwa, ameibua hisia kali bungeni leo Mei 21, 2026 baada ya kuzungumza kwa uchungu mkubwa kuhusu hali mbaya ya barabara na huduma za miundombinu katika Mkoa wa Mara wakati akichangia Bajeti ya Wizara ya Ujenzi.
Katika mchango wake, Agnes Marwa ameanza kwa kumtetea Waziri wa Ujenzi Abdallah Ulega akisema ni mmoja wa mawaziri wachapakazi wanaopita wilaya kwa wilaya na jimbo kwa jimbo kufuatilia miradi ya maendeleo licha ya kukabiliwa na ukosefu wa fedha za kutosha.
Hata hivyo, Mhe. Agnes amesema pamoja na jitihada hizo, Mkoa wa Mara umeendelea kubaki nyuma katika suala la miundombinu jambo ambalo limewaumiza wananchi na viongozi wake.
Kwa sauti ya huzuni, Mhe. Agnes Marwa aliililia Serikali kuiangalia kwa jicho la huruma barabara ya Musoma,Makojo,Busokelo akisema ni moja ya maeneo yaliyosalia nyuma licha ya ahadi ya kuunganisha wilaya zote kwa barabara zinazopitika mwaka mzima.
Amesema yeye kama mwananchi wa Musoma anaumia kuona kilomita 52 pekee zikisababisha wananchi waendelee kuishi katika mateso ya vumbi na adha kubwa ya usafiri.
“Jamani tuoneeni huruma kwenye hii kilomita 52,” amesema kwa uchungu huku akisisitiza kuwa Mkoa wa Mara unastahili kuthaminiwa zaidi kutokana na historia yake ya kuwa nyumbani kwa Baba wa Taifa Julius Kambarage Nyerere na Muasisi wa Taifa hili.
Mhe. Agnes amegusia kwa maumivu hali ya madaraja ya Nyasaungu na Subuti, akisema miundombinu hiyo imekuwa ikihatarisha maisha ya wananchi na viongozi wanaopita katika maeneo hayo.
Ameeleza kuwa hata Mkuu wa Mkoa aliwahi kulazimika kushuka kwenye gari na kutembea kwa miguu kutokana na ubovu wa daraja hilo, jambo alilosema linaonyesha ukubwa wa tatizo lililopo.
Katika sehemu nyingine ya mchango wake, Mhe. Agnes Marwa amesema barabara ya Tarime ni muhimu kwa uchumi na utalii lakini bado ipo katika hali mbaya kiasi kwamba hata msafara wa Waziri Ulega uliwahi kupata pancha kutokana na ubovu wa barabara hiyo.
Kwa hisia kali, Mhe. Agnes amesema wabunge wa Mkoa wa Mara walifika hatua ya kukaa pamoja na kulia kutokana na namna wanavyochekwa na wabunge wengine kwa sababu ya hali mbaya ya miundombinu katika mkoa wao.
“Tulijifungia pamoja wabunge wa Mkoa wa Mara tukalia,” amesema huku akieleza kuwa wananchi wa Mara wanaendelea kuumia licha ya mchango mkubwa wa mkoa huo katika historia ya Taifa.
Mhe. Agnes pia ameibua kilio kuhusu Hospitali ya Rufaa ya Kwangwa ambayo amesema Serikali ya Samia Suluhu Hassan imewekeza fedha nyingi kuijenga, lakini bado wananchi wanashindwa kufika kwa urahisi kutokana na ubovu wa barabara zinazoelekea hospitalini hapo.
Amesema hata wakati wa ziara ya viongozi wa kitaifa katika hospitali hiyo, baadhi ya magari yalipata changamoto njiani kutokana na hali mbaya ya miundombinu, hali aliyosema inaendelea kuwanyima wananchi huduma bora licha ya uwepo wa hospitali hiyo kubwa ya Rufaa.

Comments
Post a Comment