TANGA imepiga hatua nyingine kuelekea kuwa kitovu kikubwa cha biashara na usambazaji wa mafuta katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati, baada ya Kampuni ya Ushauri ya Worley Consulting Group kutoka Uingereza kukabidhiwa rasmi eneo litakalofanyiwa upembuzi yakinifu kwa ajili ya ujenzi wa kiwanda cha kusafisha mafuta (Refinery) na miundombinu ya kuhifadhia nishati hiyo.
Makabidhiano hayo yaliyofanyika Leo Oktoba Mosi katika eneo la Chongoleani jijini Tanga, yameongozwa na Timu ya Pamoja ya Kitaalamu (JTT) kutoka Tanzania na Uganda, ikiwa ni mwendelezo wa ushirikiano wa kimkakati kati ya nchi hizo mbili wenye lengo la kuimarisha usalama wa nishati na kurahisisha usambazaji kwa nchi zisizo na bandari.
Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo, Kamishna Msaidizi wa Mkondo wa Kati na Chini wa Mafuta kutoka Wizara ya Nishati (Tanzania), Grace Mwakasege, alisema mradi huo utaipandisha hadhi Tanga kuwa kituo kikuu cha kupokea, kuhifadhi, na kusambaza bidhaa za mafuta kikanda.
“Miundombinu inayopendekezwa itahusisha ujenzi wa matanki makubwa ya kuhifadhi mafuta, gati maalumu la kupokelea mafuta, pamoja na bomba jipya litakalounganisha Chongoleani hapa Tanga na Kampala nchini Uganda,” alisema Mwakasege.
Aliongeza kuwa utafiti huo wa Worley Consulting Group utabaini ustahimilivu wa eneo hilo na kuainisha mahitaji yote ya kitaalamu kabla ya mradi kuanza, jambo litakalofungua fursa za ajira na ujuzi kwa Watanzania.
Kwa upande wake, Kamishna Msaidizi kutoka Wizara ya Nishati na Maendeleo ya Madini ya Uganda, Mhandisi Geoffrey Ogwang, alieleza kuwa tukio hilo ni kielelezo cha uhusiano wa kihistoria usiotetereka kati ya mataifa hayo mawili.
“Tumekuja kukabidhi eneo hili kwa mshauri ili aweze kuanza mara moja utafiti wa awali wa uwezekano wa kutekeleza mradi huu mkubwa na muhimu kwa mataifa yetu,” alisema Mhandisi Ogwang.
Akifafanua zaidi kuhusu kazi itakayofanywa na mshauri huyo, Mjumbe wa Timu ya Pamoja ya Kitaalamu, Mhandisi Aristides Katto, alisema utafiti huo utahusisha masuala ya kijioteknolojia (Geotechnical studies) kupima ardhi.
"Baada ya tafiti hizi, mshauri atawasilisha ripoti kamili kwa Timu ya Pamoja ya Kitaalamu kwa ajili ya mashauriano ya kina na kutoa maamuzi kabla ya hatua za ujenzi kuanza," alisema Mhandisi Katto.
Ujenzi wa miundombinu hii mipya unaongeza thamani ya eneo la Chongoleani, ambalo tayari ndilo kituo kikuu cha kupokelea mafuta ghafi cha Mradi wa Bomba la Mafuta la Afrika Mashariki (EACOP) lenye urefu wa kilomita 1,447 kutoka Hoima nchini Uganda.
Timu ya Pamoja ya Kitaalamu (JTT) inayosimamia mchakato huu inaundwa na maofisa kutoka Wizara ya Nishati (Tanzania), Wizara ya Nishati na Maendeleo ya Madini (Uganda), Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Shirika la Taifa la Mafuta Uganda (UNOC), wataalamu wa sheria, na wadau wengine muhimu.










Comments
Post a Comment