Wataalamu wa Sekta za Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (SMT) na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) wamekutana jijini Dodoma, kwa ajili ya kujadili namna bora ya kuimarisha ushirikiano katika sekta zao ikiwa ni pamoja na Kombe la Muungano.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kikao cha Wataalamu hao, tarehe 1 Oktoba 2026 Jijini Dodoma Mkurugenzi wa Sera na Mipango wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo (SMT), Abel Philipo, amesema kuwa Kombe la Muungano lina umuhimu katika kuimarisha umoja na mshikamano na uhusiano wa wananchi wa Tanzania Bara na Zanzibar kupitia michezo.
"Tunahitaji kulitazama suala hili kwa mtazamo mpana zaidi ya mashindano ya michezo kwa kuzingatia nafasi yake katika kuimarisha muungano, kukuza vipaji, kuongeza fursa kwa vijana na kujenga mahusiano ya karibu kati ya taasisi na wadau wa michezo kutoka pande zote mbili" alisistiza Bw. Abel.
Amebainisha kuwa, katika kikao hicho watajadili masuala mbalimbali ikiwemo maandalizi ya Mashindano ya 74 ya Ulimbwende wa Dunia ya mwaka 2027 na uhamasishaji pamoja na uelimishaji wananchi kuhusu fursa zitakazotokana na mashindano hayo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Idara ya Sera, Mipango na Utafiti wa SMT Ndg. Khamis Khamis amesema kuwa kikao hicho kitatekeleza yale ambayo yataazimiwa kwa ustawi wa sekta hizo.
Aidha, amesema kuwa kupitia kikao hicho wanatarajia kuongeza maeneo mapya ya ushirikiano kwa ajili ya kukuza sekta zao na kuchangia maendeleo ya nchi.


























Comments
Post a Comment