Na Mashaka Mhando, Arusha
MBUNGE na mmoja wa 'Wabunge Vinara', Mhandisi Mwanaisha Ulenge, ameishauri Serikali kutunga Sheria ya Ufuatiliaji na Tathmini (M&E) badala ya kuishia kuunda vitengo pekee, huku akisisitiza lengo la Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050 lazima liwe jumuishi na kumhakikishia kila mwananchi pato la Dola 7,000.
Mhandisi Ulenge ametoa kauli hiyo mjini Arusha wakati akizungumza kwenye Kongamano la Tano la Wiki ya Ufuatiliaji na Tathmini, lililoandaliwa na Ofisi ya Waziri Mkuu, lenye lengo la kuimarisha utamaduni wa kufuatilia na kutathmini miradi ya maendeleo.
Katika hotuba yake iliyolenga kusukuma maendeleo yanayomjali mtu, Mbunge huyo alisema matamanio ya Wabunge Vinara ni kuona rasilimali za Taifa zinaleta maendeleo halisi yanayoboresha maisha, kulinda utu, na kuzalisha fursa kwa wananchi.
"Tunatamani malengo ya Dira ya 2050 ya kufikia uchumi wa Dola Trilioni 1 iende sambamba na kuhakikisha pato la mwananchi mmoja mmoja la Dola 7,000 linafikiwa. Sina mashaka sana na Serikali kufikia uchumi wa Dola Trilioni moja; mashaka yangu ni kiasi gani uchumi huo utakuwa jumuishi kufikia hilo pato la Dola 7,000 kwa mwananchi ifikapo 2050," alihoji Mhandisi Ulenge.
Pamoja na changamoto hiyo, Mbunge huyo aliipongeza Serikali kwa hatua kubwa iliyochukua ya kuanzisha Vitengo vya Ufuatiliaji na Tathmini katika Taasisi zote za Umma hadi Serikali za Mitaa, sambamba na kuandaa miongozo kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu, akitaja hatua hiyo kuwa ni muhimu kuelekea utekelezaji wa dira hiyo.
Akitoa ushauri kwa Serikali ili kufikia malengo hayo kwa ufanisi, Mhandisi Ulenge alisema kuanzishwa kwa vitengo hivyo pekee haitoshi, bali Taifa linahitaji kuwa na Sera rasmi ya Ufuatiliaji na Tathmini ambayo hatimaye itazaa Sheria kamili itakayosimamia na kubana matumizi ya rasilimali kisheria.
Aidha, alishauri miongozo iliyoandaliwa isambazwe na kufikishwa moja kwa moja kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa huko chini kwani ndiko miradi inakotekelezwa, ili kuwapa wananchi tabasamu.
Aliongeza kuwa kuna uhitaji wa haraka wa kuwa na mfumo jumuishi utakaounganisha taarifa zote za ufuatiliaji nchi nzima.
Mhandisi Ulenge alihitimisha kwa kusisitiza kuwa jambo lolote litakalofanyika katika kupanga na kutathmini miradi ya maendeleo, lazima mwananchi awe katikati ya mipango hiyo ili kuchagiza uboreshaji wa maisha yake ya kila siku.









Comments
Post a Comment