Na. Wellu Mtaki, Geita
KAMPUNI ya kizawa ya Tanzania inayojihusisha na usambazaji wa vilipuzi na huduma za ulipuaji katika sekta ya madini, ESAP, imeendelea kuwekeza katika teknolojia na mitambo ya kisasa kwa lengo la kuongeza uwezo wa kutoa huduma kwa migodi mikubwa, ya kati na wachimbaji wadogo nchini.
Uwekezaji huo umeifanya kampuni hiyo kuongeza ushiriki wake katika mnyororo wa thamani wa sekta ya madini, huku ikipanua huduma zake katika maeneo mbalimbali yanayojihusisha na shughuli za uchimbaji nchini.
Akizungumza mkoani Geita wakati wa Maonesho ya Teknolojia ya Madini, Mkurugenzi wa ESAP, Yahya Puyaga, alisema uwekezaji katika teknolojia ya kisasa umeiwezesha kampuni hiyo kukidhi mahitaji yanayoongezeka katika sekta ya madini.
“Local content imetuwezesha sisi kufika na kutoa huduma katika sehemu mbalimbali. Tumewekeza katika teknolojia ya kisasa na mitambo inayotuwezesha kutoa huduma kulingana na mahitaji ya sekta ya madini,” alisema Puyaga.
Alisema tofauti na baadhi ya kampuni zinazojihusisha na biashara ya usambazaji wa vilipuzi katika Afrika Mashariki ambazo zina asili ya nje ya nchi, ESAP ni kampuni ya kizawa inayomilikiwa kwa asilimia 100 na Watanzania.
Kwa sasa, kampuni hiyo inasambaza vilipuzi katika baadhi ya migodi nchini, ikiwemo Bulyanhulu, STAMIGOLD na Shanta, sambamba na kutoa huduma za ulipuaji katika maeneo mbalimbali ya migodi.
Puyaga alisema katika kuongeza uwezo wa uzalishaji, ESAP imewekeza pia katika kiwanda kilichopo Wilayani Bukombe, ambacho kinasaidia kuongeza uwezo wa kuzalisha bidhaa zinazohitajika katika shughuli za uchimbaji.
Aidha, alisema kampuni hiyo imeagiza magari maalumu yenye teknolojia ya kuchanganya vilipuzi katika maeneo ya migodi, hatua inayolenga kuongeza ufanisi na kuboresha utoaji wa huduma katika maeneo ya uchimbaji.
Kwa mujibu wa Puyaga, uwekezaji huo ni sehemu ya utekelezaji wa dhana ya local content, kwa kuwa unatoa nafasi kwa Watanzania kushiriki zaidi katika shughuli za uzalishaji na utoaji wa huduma zinazohusiana na sekta ya madini.
Alisema kampuni hiyo pia inalenga kuhakikisha wachimbaji wadogo wanapata bidhaa na huduma zinazokidhi mahitaji yao, hasa kutokana na kuongezeka kwa shughuli za uchimbaji wa chini ya ardhi (underground mining).
“Tunataka bidhaa hizi zipatikane kwa kiwango kinachohitajika ili kuwasaidia wachimbaji wadogo kupata huduma na vifaa kwa gharama nafuu zaidi, huku viwango vya teknolojia na usalama vinavyotakiwa katika sekta ya madini vikizingatiwa,” alisema.
Uwekezaji huo unaelezwa kuwa sehemu ya juhudi za kuongeza ushiriki wa kampuni za Kitanzania katika mnyororo wa thamani wa sekta ya madini, badala ya kutegemea zaidi huduma na bidhaa kutoka nje ya nchi.

Comments
Post a Comment