Kampuni ya Kizalendo ESAP Yawekeza Kiwanda cha Vilipuzi Bukombe Kuhudumia Migodi Mikubwa na Wachimbaji Wadogo
Mafanikio ya Sera ya Maudhui ya Ndani (Local Content) katika sekta ya madini yameanza kuonekana wazi baada ya kampuni ya kizalendo ya ESAP Mining Services kuwekeza kiwanda cha kisasa cha uzalishaji wa vimiminika vya vilipuzi Wilayani Bukombe.
Mkurugenzi wa kampuni hiyo, Mhandisi Yahya Ruyaga, akizungumza Oktoba 2, 2026 katika Maonesho ya 9 ya Kitaifa ya Teknolojia ya Madini yanayoendelea katika Viwanja vya Dkt. Samia Suluhu Hassan mkoani Geita, amesema uwekezaji huo unalenga kupunguza utegemezi wa kuagiza vilipuzi kutoka nje na kuhakikisha huduma hiyo inapatikana kwa urahisi nchini.
"Kupitia kiwanda chetu cha Bukombe tunazalisha vimiminika maalumu vinavyotumika kwenye mifumo ya vilipuzi na tunatumia magari maalumu yenye teknolojia ya kuchanganya vilipuzi moja kwa moja eneo la kazi. Hii inaongeza usalama na ufanisi," amesema Ruyaga.
Ruyaga amesema licha ya kuhudumia migodi mikubwa kama Bulyanhulu, Shanta Mining, Siam Gold na Nyanzaga, nguvu kubwa ya kampuni yake sasa imeelekezwa kwa wachimbaji wadogo na wa kati katika Ukanda wa Ziwa ambao kwa muda mrefu wamekosa teknolojia rafiki na nafuu.
Amebainisha kuwa kampuni yake ipo kwenye mazungumzo na kampuni za kimataifa kupata mashine ndogo za kisasa zitakazoweza kutumika kwenye uchimbaji wa chini ya ardhi, hatua itakayopunguza gharama kwa wachimbaji wadogo.
"Mashine hizo zikija zitakuwa mkombozi kwa wachimbaji wa chini ya ardhi. Tunataka teknolojia ifike kwa mchimba mdogo pia, si kwa mgodi mkubwa pekee," alisema.
Mhandisi Ruyaga ameishukuru Serikali kupitia Wizara ya Madini kwa kuweka mazingira wezeshi ya uwekezaji ambayo yamewezesha kampuni za wazawa kama ESAP kuwekeza kwenye teknolojia na uzalishaji wa ndani, jambo linaloongeza ushiriki wa Watanzania katika mnyororo mzima wa thamani ya madini.

Comments
Post a Comment