Na Mwandishi wetu,Musoma.
Katibu Mkuu Mtendaji wa Amani na Maendeleo Organization (AMO) Jovina Massano ashauri umuhimu wa kuimba wimbo wa Taifa katika mikutano,majukwaa na makongamano mbalimbali ili kukuza uzalendo nchini.
Ushauri huo umetolewa katika jukwaa la Mwaka la mashirika yasiyo ya kiserikali NGOs lililoyakutanisha mashirika yaliyopo mkoani Mara katika ukumbi wa uwekezaji uliopo katika ofisi ya Mkuu wa mkoa wakati wa majadiliano mbalimbali.
Jukwaa hilo limehudhuliwa na Msajili msaidizi ngazi ya Taifa kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, wanawake na makundi maalum, viongozi wa mkoa, wilaya wakiwemo wajumbe wa Baraza la Taifa la NGOs na kuongozwa na mgeni rasmi mkuu wa mkoa huo Brigedia Jenerali Evans Mtambi ambae ndie Mwenyekiti wa jukwaa hilo.
Jovina ametoa ushauri huo wakati wa majadiliano ambapo amewaomba viongozi kuhakikisha wimbo wa Taifa unakuwa sehemu ya kwanza ya ratiba ya shughuli zinazoikutanisha jamii hasa katika mikutano,warsha,bonanza,michezo ,matamasha, majukwaa na makongamano ili jamii iweze kutambua umuhimu wa uzalendo kwa nchi yetu na kudumisha Amani.
"Uimbaji wa wimbo wa Taifa mara kwa mara utahamasisha uzalendo kwa jamii nzima na kutambua umuhimu wa kulinda amani kwa Maendeleo ya Taifa,uwekwe utaratibu rasmi kuanzia ngazi ya mtaa,kata,Wilaya, mkoa,Taifa kwenye vikao vya taasisi za serikali na taasisi binafsi pia mikutano ya vikundi vya uzalishaji mbalimbali hii italeta chachu ya kutunza amani," amesema Jovina.
AMO imeunga mkono wimbo wa Hello Tanzania ulioimbwa na Vijana wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT)Rwamkoma uliotambua juhudi za serikali katika kuchochea Maendeleo kwa Taifa kuwa wimbo mojawapo maalum utakaokwenda kutumika kwenye shughuli za hamasa kwa kutambua hatua za kimaendeleo nchini.
AMO inaamini wimbo wa Taifa kuibwa Mara kwa mara itawezesha kurithisha uzalendo kwa vizazi vya sasa na vijavyo huku jamii ikipata hamasa ya kulitunza Taifa na kuiendeleza misingi ya amani,Upendo na mshikamano kwa watanzania.
Ulindaji wa misingi hii ni kuonyesha heshima na nidhamu kwa waasisi wa Taifa na uthamini unaopelekea kuheshimiana kwa kuzingatia maslahi ya Taifa.
Jukwaa hilo limebeba ujumbe wa kuzihitaji NGOs kuwa na Fikra mpya kuhusu uendelevu wa mashirika yasiyo ya kiserikali katika ubunifu,ubia na upatikanaji wa rasilimali fedha kupitia vyanzo vya ndani.
Hii itawezesha NGOs kujitegemea hata kama kuna changamoto za kuifadhili Kutoka kwa wafadhili wa nje miradi itaendelea.
Mwenyekiti Wa jukwaa hilo Brigedia Jenerali Evans amezitaka NGOs kubuni vyanzo vya ndani vya mapato vitakavyoyawezesha kuwa na uendelevu wa utoaji huduma kwa jamii.
"Uandaaji wa maandiko mradi yenye tija yanayokwenda sambamba na uhitaji wa taasisi za ndani kuna uwezekano mkubwa wa kupata ufadhili," amesema Jenerali Evans.
Aidha amezitaka NGOs kuwa na utekelezaji wa miradi inachochea Maendeleo kwa jamii nchini inayokwenda na Dira ya Taifa ya mwaka 2050.
Kwa Upande wake Mkurugenzi wa Shirika la Hope for Girls and Women in Tanzania, Rhobi Samwelly ambaye ni Mjumbe wa Baraza la Taifa la NGOs Mkoa wa Mara wakati akitoa salamu za Baraza hilo katika Jukwaa hilo amesema mashirika mengi hivi sasa yanakabiliwa na changamoto za kifedha katika kutekeleza miradi.
Kutokana na hali hiyo amezishauri NGOs kubuni vyanzo vya mapato vya ndani ili ziweze kuendelea kuhudumia jamii kwa kuwa wafadhili wengi wa nje kwa sasa wamesitisha na kupunguza misaada kwa mataifa yanayoendelea.
Pia amezisisitiza NGOs kushirikiana kwa pamoja na kujenga ubia madhubuti na Serikali, taasisi za kifedha, wadau wa maendeleo pamoja na wananchi ili kufikia malengo tarajiwa.
Msajili msaidizi ngazi ya Taifa kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, wanawake na makundi maalum, Patrick Mafuru amezikumbusha NGOs kufuata taratibu na sheria zinazowasimamia ikiwemo ulipaji wa ada kwa wakati na kuwasilisha taarifa kupitia mfumo.



Comments
Post a Comment