Na Wellu Mtaki, Geita
Kampuni ya Yetu Motors imewataka Watanzania wanaopanga kuagiza magari kupitia mitandao kuwa makini na gharama na changamoto zinazoweza kujitokeza wakati wa mchakato wa ununuzi na usafirishaji wa magari kutoka nje ya nchi.
Yetu Motors imesema kuagiza gari mwenyewe kupitia mitandao si jambo baya, lakini mteja anapaswa kufahamu kuwa anapochagua kufanya hivyo, anakuwa na wajibu wa kushughulikia changamoto mbalimbali zinazoweza kujitokeza katika mchakato huo.
Kwa mujibu wa kampuni hiyo, miongoni mwa changamoto zinazoweza kujitokeza ni mabadiliko ya gharama wakati wa mchakato wa uagizaji na usafirishaji, ambapo gharama ambazo mteja alizikadiria wakati wa kununua gari zinaweza kuongezeka kutokana na sababu mbalimbali.
Yetu Motors imesema tofauti na mteja anayeagiza gari mwenyewe, kampuni hiyo inabeba wajibu wa kushughulikia changamoto zinazoweza kujitokeza katika mchakato wa usafirishaji wa gari hadi kumfikia mteja.
Aidha, kampuni hiyo imeeleza kuwa changamoto nyingine inaweza kujitokeza wakati wa gari kuhamishwa kutoka bandari kuu kwenda bandari ya nchi kavu au katika hatua nyingine za usafirishaji.
Imeelezwa kuwa endapo gari lililoagizwa na mtu binafsi litapata hitilafu katika hatua hizo, gharama za matengenezo zinaweza kuwa jukumu la mmiliki mwenyewe.
Hata hivyo, Yetu Motors imesema gari linapoagizwa kupitia kampuni hiyo, endapo litafika likiwa na hitilafu, kampuni haitamkabidhi mteja gari hilo bila kwanza kushughulikia tatizo hilo, huku gharama za matengenezo zikiwa jukumu la kampuni kwa mujibu wa masharti yao ya huduma.
Kampuni hiyo pia imeonya kuhusu changamoto zinazoweza kugundulika baada ya gari kununuliwa. Imeelezwa kuwa wakati mwingine ukaguzi wa gari unaofanyika nchini Japan unaweza kuonyesha gari likiwa katika hali nzuri, lakini baada ya mchakato wa ununuzi kukamilika, mteja anaweza kugundua baadhi ya kasoro au vitu ambavyo havikukamilika.
Kwa mtu aliyeagiza gari mwenyewe, Yetu Motors imesema gharama zinazotokana na changamoto kama hizo zinaweza kuwa jukumu lake mwenyewe.
Kwa upande mwingine, kampuni hiyo imeeleza kuwa lengo la huduma yake ni kumpunguzia mteja mzigo wa kushughulikia changamoto zinazoweza kujitokeza katika mchakato wa kuagiza gari, kuanzia uchaguzi wa gari, ununuzi, usafirishaji hadi gari kumfikia mteja.
Yetu Motors imesema baadhi ya Watanzania huamini kuwa kuagiza gari moja kwa moja kupitia mtandao ni njia ya kupunguza gharama, lakini imewataka wateja kuangalia gharama na hatari zinazoweza kujitokeza katika mchakato mzima badala ya kuangalia bei ya gari pekee.
Kampuni hiyo imefafanua kuwa katika huduma zake, inalenga kumsaidia mteja kupata gari linalokidhi mahitaji yake kwa gharama zinazoweza kudhibitiwa, huku baadhi ya gharama zikitokana moja kwa moja na muuzaji wa gari.
Aidha, Yetu Motors imesisitiza kuwa kazi yake si kuagiza magari pekee, bali pia kutoa elimu na ushauri kwa mteja kabla ya kufanya uamuzi wa kununua gari.
Kampuni hiyo imewataka Watanzania kuepuka kufanya maamuzi kwa kufuata tamaa au kuona tu gari ambalo mtu mwingine anatumia na kutaka kuwa nalo bila kwanza kuzingatia matumizi yake, hususan gharama za mafuta, matengenezo na mahitaji mengine ya gari hilo.
Kwa mujibu wa Yetu Motors, lengo ni kuhakikisha mteja anafanya uamuzi sahihi na kupata gari linaloendana na mahitaji na uwezo wake, huku akipata usalama zaidi katika mchakato wa uagizaji.



Comments
Post a Comment